Mbeya City yapata ushindi wa kwanza VPL

Baada ya kumaliza michezo saba na kutoka sare mbili na kufungwa mitano hatimaye Mbeya City imeonja ladha ya ushindi baada ya kushinda mabao 2-1 wakiwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar.

Mabao ya washindi yalifungwa na Abdulrazack Mohammed kwa penalti dakika ya pili kabla ya Siraji Juma kuongeza la pili dakika ya 24.

Bao Kagera Sugar ikipata bao la kufutia machozi dakika ya 46 kupitia kwa Erick Kyaruzi baada ya kupigwa free kick.

Mbeya City imefikisha alama tano ikitoka mkiani mwa msimamo wa Ligi baada ya michezo nane.

Mechi nyingine iliyochezwa jioni ya leo ni Coastal Union dhidi ya Gwambina FC na kumalizika kwa bao 1-1.

Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema ana kazi ya kuinoa safu yake ya ulinzi ili iweze kulingana na ya ushambuliaji.

Amesema sare ya bao 1-1 na Gwambina katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Mkwakwani imemuumiza kwa sababu hakukuwa na sababu ya Gwambina kusawazisha.

"Tumeona safu ya ulinzi inahitaji nguvu ya ziada kuinoa nimeona makosa nitasahihisha na mechi ijayo naamini haitajirudia" alisema Mgunda.

Katika mchezo huo Coastal Union ilikuwa ya kwanza kuliona lango la Gwambina dakika ya pili lililotowa wavuni na Yusuph Soka aliyepigiwa krosi na Issa Abushehe

Dakika ya 14, Gwambina walikosa bao la penaltI iliyoamriwa na mwamuzi Mbaraka Rashid kutoka Arusha kutokana na Meshack Abraham kufanyiwa madhambi eneo la hatari lakini Yusuph Gunia alipiga shuti lililoambaa nje ya goli.

Dakika ya 32 Meshack Abraham aliipatia Gwambina bao la kusawazisha baada ya kitokea piga nikupige katika eneo la hatari la lango la Coastal Union.