Mbeya City yapania kufuta uteja kwa Prisons

Friday January 12 2018

 

By Godfrey Kahango

Mbeya. Mbeya City imesema mechi yake dhidi ya Tanzania Prisons ni muhimu kwao kwa mambo makuu mawili, kurudisha heshima kutoka kwa watani wao hao na pili kupata pointi tatu.

Kocha Mkuu wa City, Ramadhani Nswanzurwimo alibainisha hilo jana Alhamisi baada ya kumalizika kwa mazoezi yao waliyofanyia Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya huku akitamba kwamba hawaigopi Prisons ila inawaheshimu.

“Historia inaonesha kwa miaka mitatu mfuliluzo Mbeya City imekuwa daraja kwa Prisons, hivyo tunategemea hivi sasa ni wakati wetu kugeuza behewa. Tumefanya mazoezi ya kutosha, wachezaji wanajituma sana na makosa ya huko nyuma tumeyaona na kuyafanyia kazi. Prisons tunawaheshimu sana lakini hatuwaogopi kwani ni timu zilivyo timu nyingine za ligi kuu,”alisema kocha huyo Mrundi.

Alisisitiza kwamba mechi ya Jumapili ni muhimu kwake kwani ndio ‘Derby’ yake ya kwanza kukutana hivyo amewajenga vizuri kisaikolojia vijana wake huku akijivunia kipa wake tegemeo Owen Chaima kwani amemaliza kutumikia kifungo chake.

Aliwataka mashabiki na wadau wa City kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao huku akiamini lazima kutakuwa na mabadiliko ndani ya klabu hiyo kuanzia mechi hiyo dhidi ya Prisons.

Kocha  Nswanzurwimo alisema bado klabu yake ina nafasi kubwa kufanya vizuri katika ligi kwani katika msimamo timu hazijapishana pointi nyingi, hivyo mechi ya Jumapili ni muhimu kwake kushinda ili kusogea mbele zaidi.