Mbeya City taa nyekundu imeanza kuwaka

KUNA msemo kwamba siku njema huanza kuonekana tangu asubuhi, lakini kwa siku mbaya bila shaka nayo huanza kuonekana mapema tu hasa mtu anapoamka.

Kipute cha Ligi Kuu kimeanza tangu Septemba 6 huku Simba, Yanga na Azam FC zikipambana kileleni mwa msimamo wa ligi katika kuwania ubingwa wa msimu huu.

Wakati Bigirimana Blaise akiwa mchezaji wa kwanza kupiga bao msimu huu baada ya ushindi walioupata Namungo kwa bao hilo dhidi ya Coastal Union, Mbeya City ilikuwa timu ya kwanza kupokea kichapo kikubwa ilipolala 4-0 mbele ya KMC.

Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam iliishuhudia KMC ikipata mabao yake kupitia Emmanuel Mvuyekure dakika ya 22, Hassan Kabanda dakika ya 39, Abdul Hillary dakika ya 56 na Paul Peter dakika ya 74.

Mbeya City imeanza kwa unyonge mkubwa msimu huu ukiwa mwendelezo mbovu wa mwisho wa msimu uliopita ikibaki kwenye ligi hiyo kupitia mgongo wa nyuma baada ya ushindi wa jumla wa mabao 2-1 dhidi ya Geita Gold hatua ya mtoano na timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Wanakoma Kumwanya hao wanapaswa kurudisha morali ya wachezaji wake maana hata usajili uliofanywa unaonekana wachezaji hawana maajabu.

Mbeya City imecheza michezo mitano, haijapata ushindi hata mmoja zaidi ya kuambulia suluhu dhidi Tanzania Prisons.

MSIKIE KOCHA

Baada ya kichapo cha KMC kocha wa Mbeya City, Amri Said ‘Stam’ alisema kipigo cha mabao 4-0 walichokipata kimetokana na udhaifu wa safu yake ya ulinzi hivyo atayafanyia kazi mapungufu ili warejee wakiwa vizuri zaidi mechi zijayo.

Mbeya City imekuwa timu ya kwanza kwenye Ligi kupokea kipigo kikubwa tangu Ligi hiyo ianze. Vichapo vingine walivyopokea ni 1-0 na Yanga, 1-0 na Azam, 1-0 na Namungo FC.

“Kwa kweli hatukucheza vizuri kwani safu ya ulinzi mpaka kiungo ilikuwa hovyo, pia sikuona juhudi za kipa wetu katika kuzuia baadhi ya mabao ambayo amefungwa kizembe” amesema, Stam ambaye aliahidi kuyafanyia kazi mapungufu ya kikosi chake mara baada ya kupigwa na KMC.

MBONA MAPEMA

Tangu dirisha la usajili lifungwe Agosti 31 hazikupita hata siku 15 wakati Stam akianza kukiona kikosi chake kina mapungufu jambo linatoa shaka katika safari yao ya kubaki salama kweye ligi hiyo msimu ujao.

Uongozi wa Mbeya City unatakiwa kujipanga mapema na ikumbukwe msimu ujao timu zitakazoshiriki Ligi Kuu zitapungua na kufikia 16 hivyo nguvu ya ziada inatakiwa kuifanya.

Timu hiyo ndio jicho kubwa la wapenzi wa soka jijini Mbeya, endapo itashuka basi itapunguza morali ya soka kwa asilimia kubwa kwa wakazi wa mkoa huo.

Dirisha la usajili ndio hutumika kwaajili ya kuimarisha vikosi vya timu na Mbeya City ni miongoni mwa timu zilizoingia sokoni kusaka nyota baada ya mastaa wao kadhaa kuwakimbia.

NGUVU MPYA

Ikumbukwe chama hilo hadi Agosti 31 ilikuwa imesajili nyota saba huku nane wakiwa wamemaliza mkataba na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.

Nyota wapya waliosajiliwa ni Geofrey Mwashiuya, Taro Joseph, George Sangija, Kibu Prosper, Samwel Mauru, Castor Mhagama na Babilas Chitembe.

Asilimia kubwa ya wachezaji walioondoka walikuwa kwenye kikosi cha kwanza. Wachezaji waliomaliza mkataba ni pamoja na Peter Mapunda aliyemaliza msimu uliopita na mabao 13 akiwa kinara wa kupachika mabao kwenye timu hiyo na sasa yupo Dodoma Jiji FC.

Wengine walioondoka ni kipa, Aaron Kalambo, Alex Raphael, Baraka Johnson, Mohamed Kapeta,Ally Nassoro, Samir Luhava na Mohamed Mussa.

CHUPUCHUPU

Mbeya City ilimaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya 15 ikiwa na alama 45 sawa na Mtibwa Sugar, Mbao na Alliance FC ambazo mbili zipo FDL.

Nafasi waliyoimaliza walingoja hatma yao mbele ya Geita Gold FC kwenye mtoano na kupenya kwa ushindi mwembamba baada ya kupata sare ya bao 1-1 ugenini ikashinda 1-0 nyumbani na kusalia ligi hiyo huku akiishuhudia Mbao FC ikishuka na Ihefu ikipanda

Kutokana na matokeo wanayozidi kuyapata kwenye Ligi Kuu na namna timu inavyocheza bado Stam na jeshi lake linalokazi ya ziada kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwa michezo ijayo.