Mbeya City ni shidaaa!

UKIACHANA na msimu uliomalizika ambao Mbeya City ilinusurika kushuka daraja bado inaendelea kukumbana na changamoto katika Ligi Kuu Bara kwenye mechi nne ilizocheza na haijaambulia kitu mpaka sasa.

Msimu uliopita Mbeya City iliponea chupuchupu kushuka daraja baada ya kucheza mechi ya mtoano na Geita Gold katika Uwanja wa Sokoine jijini humo, ambapo ilishinda mabao 2-1.

Oktoba 3, timu hiyo inacheza dabi na Prisons ambayo ipo nafasi ya 11, ikiwa imeshinda mechi moja, sare moja na kupoteza mbili na hivyo inamiliki pointi nne, huku Mbeya City ikiwa inaburuzwa mkia.

Kutokana na mwenendo huo, wadau wa soka wametoa mitazamo yao - kubwa zaidi wakielezea jinsi ambavyo mfumo wa timu kushuka daraja ulivyo mgumu na kwamba timu inayoanza vibaya ni rahisi kurejea Ligi Daraja la Kwanza.

Kocha wa timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’, Bakari Shime anasema kwa mfumo wa sasa ambapo zinashuka timu nne moja kwa moja na mbili kucheza mchujo ni hatari kwa Mbeya City kuwa kwenye alama nyekundu endapo itaendelea na matokeo hayo. “Ligi ya sasa ni biashara asubuhi jioni hesabu, ina maana kwamba ukijiweka kwenye mazingira mazuri katika msimamo wa ligi inakuwa rahisi mechi za mwishoni kujua zitakufikisha wapi, tofauti na kujikwamua kushuka daraja,” anasema.

Staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel anasema Mbeya City inatakiwa kujitafakari mapema ili kuweka mambo sawa kabla ya kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.

“Walikuwa na msimu mbaya ulioisha, wameanza vibaya, lazima wachezaji, viongozi na makocha wakae chini kujitathmini kujua nini wafanye ili timu irejee kwenye morali, wakiamua hakuna jambo linashindika,” anasema.

WACHEZAJI

Winga wa zamani wa timu hiyo, Raphael Daud anasema msimu wa kwanza kikosi kilikuwa moto wa kuotea mbali walikutana wachezaji wenye umri sawa waliokuwa wanasaka mafanikio ya vipaji ili kuwalipa, hivyo morali ilikuwa juu.

Daud aliitumikia Mbeya City msimu wa 2014/17, kisha alijiunga na Yanga 2017/20. Hata hivyo imeachana naye, ambapo anasema kipindi hicho timu ilitoka kupanda daraja, hivyo walikuwa na hamu ya kuonyesha kitu Ligi Kuu.

“Ukiachana nasi kuwa na umri sawa, pia mifumo ya kocha Juma Mwambusi ilitubeba. Baada ya kuondoka ni kama aliondoka nayo, pia kikosi ni mchanganyiko. Sasa sijui wanakuwa wanaambiana nini, sisi tulikuwa tunaambizana lazima tujitume ili tutoboe,” anasema.

Naye Eliud Ambokile anayekipiga TP Mazembe kwa sasa wakati anacheza Mbeya City, alikutana na wachezaji wakongwe, lakini jambo analoliamini ni bidii na moyo wa kujitolea kwa timu ikiwa kwenye mazingira yoyote.

“Wakati mwingine inakuwa ni upepo umekaa vibaya, lakini pia lazima wachezaji wapambane kwa kadri wanavyoweza kuona wanaondoka kwenye hatari ya kuwa mazingira hatarishi,” anasema.

“Nakumbuka wakati naanza kucheza niliwakuta wakongwe ambao muda mwingine walikuwa wananikatisha tamaa, lakini niliamua kusimamia ninachokiamini na sasa nipo TP Mazembe licha ya kwamba bado sijaanza kupata nafasi kikosi cha kwanza.”

NAHODHA ANASEMAJE?

Nahodha wa timu hiyo, Hassan Mwasapili anakiri kuwa wachezaji wamepoteza umakini, kwani wanapata nafasi za kufunga lakini wamekuwa hawazitumii ipasavyo na mwisho wa siku wanajikuta wakiambulia vipigo.

“Kilichochangia tuwe hapa tulipo ni umakini kupungua,” anasema.