Mbeya City mdogo mdogo tu mtawaelewa

Friday July 19 2019

 

By Mwanahiba Richard

KLABU ya Mbeya City chini ya kocha Juma Mwambusi hawana presha na usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kwani wamedai wanategemea zaidi wachezaji wao kutoka timu ya vijana.
Mwambusi ndiye aliyeipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara amerudi kuifundisha baada ya kocha Mrundi, Ramadhani Nswanzurwino kumaliza mkataba.
Mpaka sasa timu hiyo haijatangaza mchezaji hata mmoja mpya aliyesajiliwa lakini imedaiwa kuwa kuna wachezaji wanaendelea kuzungumza nao huku wengine watapandishwa kutoka U20 pamoja na wengine kuchaguliwa kupitia mchujo unaoendelea.
Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema Julai 31kikosi kizima cha timu yao kitajulikana na kuingia kambini mwezi ujao ambapo kambi hiyo itategemea na mapendekezo ya kocha wao.
Kimbe amesema wamepokea mialiko kutoka mikoa mitano hivyo itapendekezwa mkoa mmoja ambao watapiga kambi.
"Kuna mkoa wa Morogoro, Sumbawanga, Songea, Dar es Salaam na visiwani Zanzibar ambako tumealikwa lakini maamuzi yatatolewa baada ya kujadiliana na kocha wetu, tulianza maandalizi muda mrefu kwa kucheza mechi mbili za kirafiki Kanda ya Ziwa.
"Maandalizi hayo yanaendelea ingawa mwezi ujao ndipo tutaingia kambini moja kwa moja kwani hata mambo ya usajili tutakuwa tumemaliza," anasema Kimbe.
Kimbe anasema hawana hofu na usajili wao kwani hata msimu uliopita wachezaji wengi hawakuwa na majina makubwa lakini walifanya vizuri.
Msimu huu miongoni mwa nyota wanaotegemewa Mohamed Samatta na Victor Hangaya wameondoka na kutua timu zingine. Samatta amesajiliwa KMC wakati Hangaya ametua Biashara United ya Musoma.


Advertisement