Mbeya City, Prisons kazi ipo

Muktasari:

  • Akizungumza jana, kocha msaidizi wa Mbeya City Mohammed Kijuso alisema wamejipanga kuendeleza ushindi katika mchezo huo ingawa alidai haitakuwa kazi rahisi.

Mbeya. Mechi ya watani wa jadi Prisons na Mbeya City huenda ikaweka rekodi mpya zitakapovaana katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Sokoine.

Rekodi zinaonyesha tangu Mbeya City ilipopanda daraja msimu 2013/2014 imecheza na Prisons mara 12, imeibuka na ushindi mara nne, imefungwa mechi nne na imetoka sare michezo minne.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuamua nani zaidi ingawa Prisons ina deni la kulipa kisasi baada ya kufungwa mabao 2-1 katika raundi ya kwanza ya mashindano hayo msimu huu.

Akizungumza jana, kocha msaidizi wa Mbeya City Mohammed Kijuso alisema wamejipanga kuendeleza ushindi katika mchezo huo ingawa alidai haitakuwa kazi rahisi.

“Katika mchezo huu sisi ndiyo wenyeji, hivyo tutatumia fursa hiyo kuhakikisha hatupotezi mchezo huo muhimu, mchezo wa mwisho tulitoka sare na Stand United kutokana na mapungufu ya baadhi ya wechezaji lakini tumefanyia kazi kasoro zote,”alisema Kijuso.

Kocha wa Tanzania Prisons, Mohammed ‘Adolf’ Richard alisema watapambana kupata pointi tatu katika mchezo huo na ameandaa kikosi imara.

“Tutapambana kwa hali ya juu kuhakikisha hatupotezi mchezo huu muhimu kwetu, naomba mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanjani kushuhudia mchezo huu”, alisema Richard.

Mechi nyingine zinazotarajiwa kuchezwa leo ni Yanga dhidi ya Mbao na KMC itamenyana na Mtibwa Sugar.