Mbeya City, Prisons hapatoshi Dabi ya Mbeya

Muktasari:

 

  • Mbeya City inakwenda katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare Stand United, wakati Prisons ikichapa Azam

MBEYA. Sahau dabi ya Kariakoo, moto utawaka kesho katika dabi la jijini Mbeya wakati Mbeya City uso kwa uso na Tanzania Prison kwenye Uwanja wa Sokoine.

Tangu Mbeya City wamepanda Ligi Kuu mwaka 2013/14, wamekutana Prison mara 12. City imeshinda michezo minne wakifungwa minne na kutoka sare michezo minne, kesho wanakutana ukiwa mchezo wa 13.

Wakizungumza mchezo huo makocha Mohamed Kijuso wa Mbeya City na Adolf Richard wa Prisons kila mmoja amejingamba kushinda mchezo huo.

Kocha msaidizi wa Mbeya City, Kijuso alisema kikosi chake kimejipanga kisawa sawa kuwakabili mahasimu wao.

“Katika mchezo huu sisi ndiyo wenyeji hivyo tutatumia fursa hiyo kuhakikisha hatupotezi mchezo huo muhimu kwetu.

“Tulitoka sare katika mchezo wetu uliopita dhidi ya Stand United kutokana na mapungufu kwa baadhi ya wechezaji na tayari tumeyafanyia kazi hata hivyo wachezaji ambao walikuwa na matatizo ya kifamilia tunatarajia kuungana nao katika mchezo huo,” alisema Kijuso.

Kocha wa Prisons, Adolf Richard alisema siwezi kusema tutashinda au tutashindwa wala kusema chochote kwani mpira ni dakika 90.

“Tutapambana kuhakikisha hatupotezi mchezo huu muhimu kwetu cha msingi mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia mchezo huu dhidi ya watani wetu,” alisema Richard.