Mbelgiji aipigia hesabu Azam

Sunday August 11 2019

By Thobias Sebastian

KOCHA Patrick Aussems anayeinoa Simba, amesema kwa sasa amesahau kwa muda matokeo ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji waliotoka nao suluhu ugenini na akili zake amezihamishia kwenye pambano lao la Ngao ya Jamii litakalopigwa Jumamosi ijayo.

Mechi hiyo ya kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara utachezwa Uwanja wa Samora, mjini Iringa na Kocha Aussems amsema mara baada ya kumaliza mechi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ugenini akili zake zimeama huko.

"Kabla ya kucheza na UD Songo mechi ya marudiano tutakuwa na mechi na Azam hiyo ndio ambayo tunaifikiria kwa sasa," amesema.

"Utakuwa mchezo mzuri na mgumu kwa timu zote mbili kutokana na maandalizi ambayo wamekuwa wakifanya hata ukubwa wa timu," amesema na kuongeza;

"Kikubwa tumeanza kupiga mahesabu ya kucheza nao kwa maana aina ya mchezo utakavyokuwa, na jinsi gani tunaweza kupata matokeo mazuri dhidi yao," amesema Aussems.

Katika hatua nyingine zimepatikana habari za chini ambazo hazijathibitishwa kuwa, huenda pambano hilo likahamishiwa jijini Dar es Salaam kutoka Iringa katika muda na tarehe ile ile, tunafuatilia kupata ukweli juu ya hili.

Advertisement


Advertisement