Mbelgiji abadili mbinu

Muktasari:

  • MBELGIJI wa Simba, Patrick Aussems amekiangalia kikosi chake na kubaini kuna majembe yanayofaa kutumika kwenye mechi za mkoani na wengine kwa michezo ya nyumbani, lengo lake likiwa ni kukusanya pointi katika Ligi Kuu Bara.

IKIWA leo Alhamisi, wiki moja kamili tangu bilionea wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji kutowekwa baada ya kutekwa na watu wasiofahamika, Kocha Mkuu wa klabu hiyo amefanya jambo moja ambalo litawapa shangwe mashabiki wa Msimbazi.

Kwa wale mashabiki wa filamu waliotimba sana majumba ya sinema kama Avalon, Odeon, New Chox, Cameo, Starlight, Empress ama Empare kwa jijini Dar es Salaam na wale wa mikoani kama Metropole au Elite Arusha wanakumbuka zile filamu za kihindi zenye stelingi wa mjini na bushi zilivyokuwa, yaani ni kama Double Impact ya Van Damme.

Sasa unaambiwa kocha Patrick Aussems naye amekiangalia kikosi chake na kufuatilia mechi zao saba walizocheza mpaka sasa katika Ligi Kuu Bara na kubaini ana wachezaji wanaofaa kucheza mechi za jijini Dar na zile za mikoani ili kupata matokeo.

Kocha huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa, katika kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mechi zao kwa viwanja vyote vinavyotumika katika Ligi Kuu Bara, kuanzia sasa atakuwa anatumia baadhi ya wachezaji kulingana na viwanja wanavyocheza.

Aussems allisema amekuwa akichukizwa na ubora wa viwanja vinavyotumika katika Ligi Kuu Bara lakini amebaini kukasirika kwake hakuwezi kumsaidia na badala yake anajipanga ili kuhakikisha hapotezi tena pointi kirahisi.

Alisema baadhi ya viwanja hasa vya mikoani vimekuwa sio rafiki kwa aina ya soka wanalocheza la kuweka mpira chini na hapo atapanga vikosi viwili kutokana na aina ya wachezaji alionao Simba ambao watazicheza mechi hizo za mikoani.

Alisema kuna aina ya wachezaji kama Meddie Kagere, Emmanuel Okwi ni wazuri wanapocheza jijini Dar es Salaam na watu kama John Bocco, Adam Salamba ama kina Marcel Kaheza ni watamu kwa mechi za mikoani na amepanga kuwatumia huko.

“Nafikiria kuanza kugawanya vikosi viwili ndani ya Simba, kimoja kitakuwa na hao wachezaji ambao watakuwa wakitumika ugenini na hasa wale waliokosa nafasi katika kikosi cha kwanza, wengine tutakuwa tunawatumia mechi za nyumbani,” alisema na kuongeza; “Siwezi kubadilisha aina ya soka letu eti kwa sababu ya viwanja Simba lazima iwe na falsafa yake ya uchezaji sipendi soka la kubutua ni lazima tucheze kwa kuweka mpira chini ndio maana najipanga kuwapa majukumu wasiopata nafasi nyumbani.”

Aussems alisema wachezaji wote walipo Simba ni wazuri na kwamba kwa mpangilio huo wa kugawana makundi mawili itasaidia kila mmoja kupata nafasi ya kucheza na kuisaidia timu kupata matokeo katika kusaka ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo.

“Shirikisho wanatakiwa kuboresha viwanja hivi, ili soka la nchi hii lipande unapokuwa ugenini nje ya Dar unapata wakati mgumu kutokana na viwanja,” alisema Aussems.

VIKOSI VILIVYO

Tangu Aussems aanze kuinoa Simba amekuwa akiwatumia baadhi ya wachezaji wake katika mechi za nyumbani na ugenini na kufanya mabadiliko kidogo, langoni huwa anakaa Aishi Manula, Shomari Kapombe, Asante Kwas/Tshalalala, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, James Kotei, Cletus Chama/Hassan Dilunga, Meddie Kagere, John Bocco/Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.