Mbelgiji Simba ataiweza rekodi Phiri

Friday July 20 2018

 

Dar es Salaam. Kocha mpya wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems ana kibarua cha kuisaka rekodi Mzambia Patrick Phiri aliyoweka msimu 2010-11, kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza mechi yote.

Tangu Phiri ameweka rekodi hiyo hakuna timu iliyofanikiwa kuivunja japokuwa msimu uliopita kocha Joseph Omog, Pierre Lechantre ilibaki kidogo waivunje kabla ya kupoteza mechi ya mwisho ya Ligi Kuu wakati Simba ilipochapwa bao 1-0 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Rekodi hiyo ya Phiri imeingia inaweza kuwa katika wakati mgumu kutokana na rekodi za kocha Aussems katika soka la Afrika aliyoweka katika Ligi Kuu ya Congo Brazzaville na Sudan.

Mbelgiji Aussems aliweka rekodi yake ya kwanza mwaka 2014 aliipa ubingwa AC Leopard ya Congo Brazzaville ikiwa mbele kwa pointi 13, haikupoteza mchezo ila timu yake ilifungwa bao moja katika msimu mzima huo.

Baada ya mkataba kumalizika alijiunga na Al Hilal ya Sudan mwaka 2015, alifanikiwa kuiongoza klabu hiyo kufuzu kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, pia hakufungwa bao lolote katika Ligi Kuu Sudan kabla ya kutimka baada ya kukwaruzana na uongozi.

Rekodi ya Aussems inaweza kumbeba kocha huyo na kufanya vyema katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Uongozi wa Simba umemtaka kocha huyo raia wa Ubelgiji kuipa ubingwa wa Ligi Kuu na kuivusha timu hiyo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Aussems amepewa mkataba wa mwaka mmoja kwa masharti ni kuipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu kiunzi ambacho anaweza kukivuka kutokana na rekodi yake kwenye ligi za ndani.

Ujio wa kocha huyo unaifanya Simba kufundishwa na makocha 10 tangu ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2011-2012 ikiwa chini ya Mserbia, Milovan Cirkovic.

Makocha waliomtangulia ni Patrick Liewig, Abdallah Kibadeni, Zdravko Logalusic, Patrick Phiri, Goran Kopunovic, Dylan Kerr, Jackson Mayanja, Joseph Omog na Pierre Lechantre.

Aussems anachukua nafasi ya Mfaransa Lechantre, aliyedumu Simba kwa miezi sita na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema wamempa kocha huyo masharti makubwa mawili ili kulinda kibarua chake.

Alisema kocha huyo atafanya kazi na kocha msaidizi, Masoud Djuma ingawa ameomba kuletewa kocha wa viungo ambaye atatangazwa hivi karibuni.

"Hadi tunaamua kufanya kazi na Patrick tuliangalia vitu vingi, makocha zaidi ya 50 waliomba kufundisha Simba, tuliwachuja na tukabaki na huyu, tulimuhoji kwa saa tano jijini Dar es Salaam," alisema Abdallah.

Aussems alisema mkakati wake ni kuifanya Simba kuwa klabu kubwa Afrika akiamini ina kikosi bora ambacho kitampa mafanikio.

Alisema anaifahamu Simba na aliwataka baadhi ya nyota anaowajua ni Emmanuel Okwi, Shomari Kapombe, John Bocco na Shiza Kichuya.

"Nawasikia wapinzani wa Simba ni Yanga na Azam, sina habari nao kwa kuwa mimi ni kocha wa Simba na malengo yangu ni kuifikisha mbali zaidi," alisema Aussems.

Advertisement