Mbelgiji Simba asaka heshima

Muktasari:

  • Kocha huyo kutoka Ubelgiji alisema safari hii wanaenda kuanza mechi yao ugenini tofauti na raundi ya awali, lakini kikubwa ni kuhakikisha wanashinda kabla ya kumaliza kazi nyumbani na kutinga makundi ambayo ndio lengo lao.

KIKOSI cha Simba kinachoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kimeshatua Zambia tayari kwa vita yao dhidi ya Nkana FC ya huko, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo Patrick Aussems amesisitiza anaenda kusaka heshima ugenini.

Simba keshokutwa Jumamosi itakuwa wageni wa Nkana kwenye Uwanja wa Nkana uliopo mjini Kitwe katika mechi ya mkondo wa kwanza wa michuano hiyo, huku ikiwa na kumbumbuku ya kuchemsha kwa wapinzani wao.

Katika mechi zao mbili zilizopita dhidi ya Nkana kwenye ardhi ya Zambia, Simba imepasuka mara zote kwa kupigwa mabao manne kila mchezo, licha ya kulipa kisasi nyumbani lakini ikajikuta mara zote iking’olewa na wakali hao.

Jambo hilo limemfanya Aussems kuondoka akiwa na tahadhari kubwa ya kuhakikisha anaenda kusaka heshima kwa kupata ushindi dhidi ya Nkana ikiwa ni mara yao ya kwanza kama watafanikiwa, huku akisisitiza hawahofii chochote kwa Wazambia.

Kocha huyo kutoka Ubelgiji alisema safari hii wanaenda kuanza mechi yao ugenini tofauti na raundi ya awali, lakini kikubwa ni kuhakikisha wanashinda kabla ya kumaliza kazi nyumbani na kutinga makundi ambayo ndio lengo lao.

“Tunaenda tukiwa na lengo letu lile lile la kushinda au kupata matokeo ambayo yatakuwa mazuri na faida kwa upande wetu kabla ya mchezo wa marudiano, ni kweli rekodi zinaonyesha hatujawahi kuifunga Nkana kwao, ila sio tatizo kwangu.”

Kocha Aussems alisema kwake anachotaka ni kushinda kila mechi au kupata matokeo bora bila kujali rekodi za mechi za nyuma, kwa sababu rekodi zinawekwa ili zivunjwe na yeye anaenda kuvunja rekodi ya Nkana dhidi ya Simba kwao.

Alisisitiza, wachezaji wake wote wana uwezo wa kucheza mpira wa kupasiana pasi ndefu au fupi, hivyo wakiwa wanazuia muda mwingi hautakuwa mfumo rafiki kwa upande wao.

Kuhusu kikosi atakachokitumia kwenye mchezo huo mgumu, Aussems alisema;

“Hakutakuwa na mabadiliko makubwa na kikosi kilichoivusha timu katika mechi za awali, ila lolote linaweza kutokea kulingana na maandalizi ya mwisho.”

BOCCO MZUKA

Naye Nahodha wa Simba, John Bocco alisema wanatambua wanacheza na timu nzuri, ambayo imefuzu katika hatua ya kwanza kama wao lakini kwa maandalizi ambayo wameyapata wanauwezo wa kupata matokeo mazuri katika mechi zote.

Bocco alisema anachoamini kocha ataweka malengo mazuri ya mechi na Nkana na kama wachezaji watapambana zaidi ya mchezo wa kwanza, itakuwa silaha kubwa kwao ili kupata ushindi au matokeo ya faida kwa upande wao.

“Wachezaji tutapambana na kufanya kazi yetu ili kuipeleka timu katika nafasi nzuri na pia tuwapongeze mashabiki, wameonekana na muamko mkubwa wa kuja Zambia na wamekuwa wakifanya hivyo hata tukicheza mechi ndani ya nchi na tunawaomba wasiache kufanya hivyo,” alisema Bocco.

REKODI

Rekodi zinaonyesha Simba na Nkana zimekutana mara mbili katika mechi za Afrika mwaka 1994 ambapo Simba ililala mabao 4-1 kisha kulipa kisasi nyumbani kwa ushindi wa mabao 2-0 ya raundi ya pili ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Mara ya mwisho tena kukutana ni raundi ya awali dhidi ya wababe hao wa Kitwe, ambapo ikianzia ugenini tena ilicharazwa mabao 4-0 kabla ya kushinda nyumbani kwa mabao 3-0.

Hata hivyo kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kimeweka msimamo kuwa hakitoi kiki.