Mbelgiji, Tambwe walianzisha mapema

Muktasari:

  • Akizungumza Mwanaspoti, Tambwe alisema Simba ni timu kubwa, lakini haina kikosi cha kuizuia Yanga isishinde mchezo huo watakapokutana, kwani safu yao ni nyepesi mno.

PRESHA na joto la homa la pambano la watani, baada ya straika mwenye bahati ya kuitungua Simba, Amissi Tambwe kulianzisha mapema, huku Kocha wa Msimbazi, Patrick Aussems akisisitiza akili yake ipo kwa Waarabu kuliko Yanga.

Simba na Yanga zitavaana wikiendi hii kwenye Uwanja wa Taifa, katika mchezo marudiano baada ya suluhu ya mchezo wa kwanza kutoka sare, lakini Kocha Aussems alisema baada ya kuinyuka Mwadui 3-0 akili yake amehamishia kwa Al Ahly.

Mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa itapigwa kesho Jumanne na Mbelgiji alisema ndio inayomuumiza kichwa kuliko Yanga akidai akishamalizana na Waarabu ndio ataanza mikakati kuelekea pambano hilo alilodai analichukulia kama mapambano mengine ya ligi.

“Dhidi ya Mwadui tulikuwa na kipindi cha kwanza kizuri ambacho tulifunga mabao, lakini tulishindwa kumaliza mechi kwa kufunga zaidi kutokana katika vichwa vya wachezaji wangu kuwa na mawazo mengi zaidi ya mechi inayofuata na Al Ahly,” alisema.

Alisema makosa yaliyojitokeza mbele ya Mwadui na hata kwenye mchezo wao wa kwanza dhidi ya Al Ahly yamerekebishwa, ili kuwanyamazisha wapinzani wao, kisha ndipo waanze kuufikiria mchezo wao ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga.

“Tukimalizana na Al Ahly ndio tutaanza maandalizi ya mechi ya Yanga, kwani malengo yetu ni kuchukua pointi tatu katika mechi zetu zote za viporo, nashukuru tumeanza na Mwadui na kushinda sasa akili yetu inaenda kwa katika mechi ya Al Ahly lengo likiwa ni kushinda pia.”

MSIKIE TAMBWE SASA

Upande wa Tambwe anayeshikilia rekodi ya kuitungia Simba mara tatu mfululizo kama ilivyo kwa Shiza Kichuya aliyetimkia Misri na mkongwe wa zamani wa Simba, Madaraka Seleman, alisema amerudi rasmi uwanjani na kwamba watani zao wajipange kwani lazima walie.

Tambwe aliumia kwenye mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Biashara United na kushonwa nyuzi tatu, huku timu yake ikipenya kwa penakti 5-4 baada ya sare ya 2-2 katika dakika 90.

Akizungumza Mwanaspoti, Tambwe alisema Simba ni timu kubwa, lakini haina kikosi cha kuizuia Yanga isishinde mchezo huo watakapokutana, kwani safu yao ni nyepesi mno.

“Tumecheza nao duru la kwanza wakiwa na kikosi hichohicho kila mmoja alipata pointi moja hawatutishi na ukizingatia wamepata matokeo mabaya katika Ligi ya Mabingwa, kilichowaangusha ni ukosefu wa nidhamu katika mabeki wao,” alisema.

“Tunafahamu mapungufu yao na ubora wao, tutavitumia kupata alama, kwani mipango yetu ni kuhakikisha tunarudi tena katika michuano ya Afrika.

Kuhusu Yanga, Tambwe alisema wanaimarika japokuwa wanakumbana na changamoto ya majeruhi kutokana na kucheza michezo mingi mfululizo.