Mbappe awavulia kofia Zidane na Cristiano Ronaldo

Muktasari:

Kylian Mbappe alisajiliwa na PSG akitokea Monaco kwa ada ya uhamisho ya Euro 145 milioni, mnamo Julai, 2018.

STRAIKA wa klabu ya Paris- Saint German (PSG), Kylian Mbappe amewataja Zinedine Zidane na Cristiano Ronaldo kuwa ndio wachezaji  wake bora wa mpira wa miguu kuwahi kuwashuhudia, aliokuwa anawaangalia kama kiigizo chake.

Mbappe ambaye alisajiliwa na PSG akitokea Monaco kwa ada ya uhamisho ya Euro 145 milioni mnamo Julai, 2018, mkataba wake wa sasa na PSG unatarajia kumalizika mwaka 2022.

 "Kwanza alikuwa ni Zidane kutokana na kile ambacho alifanikiwa kukipata kwenye timu ya Taifa alafu pia wapili ni Ronaldo ambaye ana mafanikio makubwa, lakini pia bado anaendelea kutafuta mafanikio" amesema Mbappe.

"Wote wawili wameacha alama kwenye historia ya mpira wa miguu, na mimi pia nahitaji kuacha historia yangu  kwenye mchezo huu " aliongeza

Ingawa Ligue 1 imemalizwa kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya Corona, Paris Saint-Germain bado wataendelea kucheza michezo yao ya Ligi ya mabingwa barani Ulaya iliyobakia, bila ya uwepo wa mashabiki.

"Mashabiki ni sehemu sehemu muhimu sana katika mchezo wa mpira wa miguu, kucheza mechi bila ya uwepo wao itakuwa ni jambo geni kwa wachezaji, lakini katika kupindi hiki afya zetu ni bora kuliko  kitu chochote hivyo inabidi tukubaliane na hilo ili kulinda afya zetu."

Mbappe pia alifunguka kuhusu ndoto yake ya kupata tuzo ya  Ballon d'Or  na kusema kuwa bado ana ndoto kubwa ya kushinda tuzo hiyo na haijalishi itakuwa ni baada ya muda gani.

" Itakuwa ni jambo zuri kushinda tuzo hiyo, lakini sio jambo linalonifanya mimi niamke usiku, sifikirii kwamba nahitaji kushinda katika msimu ujao ama wa kesho kutwa, hakuna ukomo wa muda niliouweka katika jambo hili nina imani kuwa naweza kushinda muda wowote"

 "Siku zote nimeiweka klabu yangu ya  PSG timu ya Taifa ya Ufaransa kama ni vipaumbele vyangu, hivyo kama tuzo binafsi zitakuja kwa upande wangu itakuwa ni ziada, lakini nafikiria zaidi kushinda nikiwa na timu sio mimi mwenyewe" amesema.