Mbappe anaendelea kuburuza ndani -nje

Friday July 12 2019

 

LONDON, ENGLAND. ANABURUZA kwa wakubwa na anaburuza kwa wadogo wenzake. Staa wa PSG, Kylian Mbappe, 20, ameendelea kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi duniani kwa sasa. Wakati akiwa mchezaji mwenye thamani kwa ujumla, sasa anawaburuza pia kwa wadogo wenzake.

Mtandao wa Soccerex umemtaja kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi chini ya umri wa miaka 21 huku ukisema ana thamani ya Euro 261.6 milioni kwa sasa ikiwa ni mara mbili ya mchezaji anayemfuatia.

Mtandao huo unaangalia zaidi umri wa mchezaji, nafasi yake, klabu yake, mkataba wake, thamani yake sokoni, mechi za kimataifa alizocheza, mabao aliyofunga, dakika alizocheza, rekodi yake ya majeraha pamoja na baadhi ya mambo mengine mengi tu.

Kwa mara ya kwanza hakuna mchezaji wa Kihispaniola katika orodha hiyo huku ikiwa ni kiashiria tosha kwamba Hispania imeanza kusuasua kuzalisha vipaji vipya tofauti na miaka michache iliyopita ambapo ilitawala katika soka duniani.

Wakati Mbappe akiburuza kwa thamani katika vipengele vyote hivyo, mchezaji aliyeshika nafasi ya pili katika orodha hiyo ni winga wa Borussia Dortmund na Timu ya Taifa ya England, Jadon Sancho, 19, ambaye thamani yake ni Euro 120.3 milioni.

Nafasi ya tatu inashikwa na beki nyota wa Ajax na Timu ya Taifa ya Uholanzi, Matthijs de Ligt, 19, ambaye dau lake limetajwa kuwa ni Euro 74 milioni. De Ligt ambaye amekuwa akitakiwa na klabu mbalimbali kubwa yuko mbioni kuhamia Juventus.

Advertisement

Nyuma ya De Ligt kuna beki mahiri wa kulia wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold ambaye thamani yake imetajwa kufikia Euro 73 milioni baada ya kuibuka kuwa mmoja kati ya wachezaji mahiri katika kikosi cha kwanza cha Liverpool kinachoongozwa na Kocha Jurgen Klopp.

Alexander-Arnold, 20, anakuwa mchezaji wa pili kwa thamani kubwa miongoni mwa wachezaji wa Kiingereza katika orodha hii ambapo wengine wanaomfuatia ni Phil Foden wa Manchester City (40.8m), Declan Rice wa West Ham (39m), Ryan Sessegnon wa Fulham (33.8m) na kinda wa Chelsea anayekuja juu Callum Hudson-Odoi (31.7m).

Kipa nambari moja wa AC Milan na Timu ya Taifa ya Italia, Gianluigi Donnarumma, 20, amesimama nyuma ya Alexander-Arnold kwa thamani akiwa na thamani ya Euro 69 milioni huku akiwa mchezaji kinda wa Italia mwenye thamani kubwa zaidi.

Anayemfuatia Donnarumma ni kinda wa kimataifa wa Brazil, Vinicius Jr ambaye anatesa katika jezi ya Real Madrid na dau lake linatajwa kufikia Euro 60 milioni ikiwa ni msimu mmoja tu tangu anunuliwe kutoka Santos ya Brazil.

Mastaa wengine makinda wenye thamani kubwa ni pamoja na Matteo Guendouzi wa Arsenal ambaye kwa sasa ametajwa kuwa na thamani ya Euro 42 milioni licha ya Arsenal kumnunua kwa dau kiduchu kutoka Lorient ya Ufaransa katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.

Staa wa Lyon, Houssem Aouar ametajwa kuwa na thamani ya Euro 41.6 milioni wakati kinda wa Timu ya Taifa ya Ufaransa, Ibrahima Konate anayekipiga katika Klabu ya RB Leipzig ya Ujerumani ana thamani ya Euro 36 milioni.

Mbrazili Rodrygo aliyenunuliwa na Real Madrid kutoka Santos ya Brazil katika dirisha hili la uhamisho ametajwa kuwa na thamani ya Euro 35 milioni.

Miongoni mwa mastaa wengine waliotajwa katika orodha hiyo ni pamoja na Nicolo Zaniolo wa AS Roma, Joao Felix aliyehamia Atletico Madrid kutoka Porto, Christian Pulisic aliyetua Chelsea akitokea Borussia Dortmund na Kai Havert wa Bayern Leverkusen.

Katika Bara la Afrika, kinda wa Nigeria, Samu Chukwueze anayekipiga katika Klabu ya Villarreal anatajwa kuwa na thamani kubwa zaidi kwa sasa akikadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Euro 30 milioni.

Chukwueze ndiye aliyefunga bao la kwanza la Nigeria katika pambano la robo fainali dhidi ya Afrika Kusini juzi Jumatano usiku katika Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazoendelea kule Misri katika pambano ambalo ‘Super Eagles’ ilishinda kwa mabao 2-1.

Advertisement