Mbappe alinusuru Ufaransa kwa Iceland

Muktasari:

Juhudi binafsi za mshambuliaji kinda wa Ufaransa Kylian Mbappe jana ziliinusuburu Ufaransa isiadhirike mbele ya Iceland, baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 hadi dakika ya 86 kabla ya kinda huyo kupika bao moja na kufunga jingine kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Guingamp, Ufaransa. Mshambuliaji chipukizi wa Ufaransa, Kylian Mbappe jana alitokea benchi kuchukua nafasi ya Antoine Griezmann katika dakika ya 60 na dakika 30 baadaye akaifungia timu yake bao la kusawazisha dhidi ya Iceland.

Katika mechi hiyo ya kirafiki iliyopigwa mjini Guingamp, na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, wenyeji walijikuta wakienda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0 baada ya Birkir Bjarnason kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 30.

Mabingwa hao wa Dunia walikianza kipindi cha pili kwa mashambulizi mazito wakiutawala mchezo lakini wakajikuta wakifungwa bao la pili dakika 58 kwa Kari Árnason kupiga kichwa maridhawa kilichojaa wavuni na kuzidi kuwaduwaza wenyeji.

Hata hivyo kuingia kwa Mbappe kuliongeza kasi ya mashambulizi na katika dakika ya 86 wakajipatia bao la kwanza lililotokana na mlinzi Holmar Orn Eyjólfsson kujifunga wakati akiokoa.

Mbappe mwenye miaka 19 mshambuliaji wa Paris St-Germain aliifungia Ufaransa bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya mwisho ya mchezo huo baada ya mlinzi mmoja kuunawa ndani ya 18.

Iwapo Iceland wangefanikiwa kushinda mchezo huo ungekuwa ushindi wao wa kwanza katika mechi dhidi ya Ufaransa kwani mara ya mwisho kukutana ilipigwa mabao 5-2 katika robo ya Fainali ya Euro 2016.

Iceland pia haijashinda mechi 12 mfululizo wakati Ufaransa nayo ikiongeza idadi ya mechi ilizocheza bila kupoteza kufikia 13 mfululizo.