Mbao yatangaza Kirumba ni machinjioni msimu huu

Muktasari:

Mbao imewatamburisha wachezaji wake sambamba na benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu, Hemed Morocco akisaidiwa na Abdulmutiki Hajji.

Mwanza. Mbao FC imetangaza hali ya hatari kwa timu za KMC, Mbeya City na Alliance FC kuwa zisitarajie mteremko katika msimu huu wa Ligi Kuu inayotarajia kuanza Jumamosi hii.

Mbao inajiandaa na mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya majirani zao Alliance FC mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kirumba jijini Mwanza.

Akizungumza leo Agosti 22 katika hafla ya kutangaza kikosi cha timu hiyo, Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Daniel Naila amesema msimu ujao timu za KMC, Mbeya City na Alliance zijiandae kwa vipigo.

Naila alisema mkakati wao katika ligi mismu huu ni kuhakikisha wanashinda mechi zote za nyumbani ambazo zitawaweka katika nafasi nzuri.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hemed Morocco alisema amesuka kikosi cha ushindani na kutamba kuwa tangu aanze kufundisha timu amepoteza mchezo mmoja wakiwa nyumbani alipokuwa akiinoa Singida United  walipochapwa bao 1-0 dhidi ya Biashara United,hivyo timu pinzani zijipange.

Naye mshambuliaji Wazir Junior alisema wamejiandaa kufanya vizuri katika mechi zao na kuwataka mashabiki kutoingilia majukumu ya benchi la ufundi badala yake watoe sapoti.

Katibu wa matawi ya Klabu hiyo, Paschal Benard amesema mashabiki watakuwa pamoja na timu yao na kuwashukuru wadau ambao wameisaidia kwa namna fulani kuibakisha timu Ligi Kuu na kwamba msimu ujao Mbao wanaitarajia kumaliza Ligi nafasi tano za juu.