Mbao yasoteshwa FDL

Muktasari:

Mbao ni miongoni mwa timu zilizoshuka daraja msimu uliopita wa 2019/20.

Mwanza. Mbao FC imeendelea kuteswa katika Ligi Daraja la Kwanza baada ya leo kupoteza mchezo wao wa tatu mfululizo dhidi ya Pamba FC kwa mabao 3-0, mechi iliyopita kwenye dimba la CCM Kirumba.

Katika mchezo huo ambao ulishuhudiwa na mamia ya mashabiki, kila timu ilihitaji ushindi lakini wenyeji Mbao walikubali kulala kwa kipondo hicho.

Alikuwa Shaban Imamu aliyeanza kuwaamsha Pamba kwa shuti kali dakika ya sita kabla ya Emanuel Haule kuiongezea bao la pili dakika ya 40 na kuwapeleka mapumziko wakiwa mbele.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana, lakini licha ya Mbao kutengeneza nafasi za mabao, straika wake walishindwa kuzitumia vyema.

Pamba ambao walicheza kwa utulivu na mashambulizi ya hapa na pale walifanikiwa kuongeza bao la tatu lililowekwa wavuni na Ajibu Ajibu dakika ya 75 na kuwafanya wapinzani kutoka mchezoni.

Kwa matokeo hayo Pamba anafikisha pointi saba, huku Mbao akibaki bila alama yoyote katika Ligi hiyo kundi B baada ya kila timu kushuka uwanjani mara tatu.