Mbao yaandika rekodi, huyo Junior ni balaa

Wednesday July 8 2020

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Mbao chini ya Kocha Mkuu, Felix Minziro imezidi kung'aa na kuandika rekodi mpya ya kucheza mechi tano mfululizo kwenye Ligi Kuu bila kupoteza.

Katika mchezo huo ambao umepigwa dimba la CCM Kirumba jijini hapa, Mbao leo ikiikaribisha Mtibwa Sugar ilishuhudiwa kandanda safi kwa timu zote kutokana na mashambulizi yaliyokuwa yakifanywa na timu hizo.

Katika mechi hiyo straika Waziri Junior  ameendelea kuonesha uwezo wake na kuisaidia timu yake kusimama imara baada ya kuipatia pointi tatu muhimu kufuatia bao lake 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kipindi cha kwanza kila timu ilifanya mashambulizi lakini ishu ya kumalizia mipira ya mwisho na kufanya kwenda mapumziko kuwa nguvu sawa ya bila kufungana.

Heka heka iliendelea katika kipindi cha pili ambapo dakika ya 64, Junior aliweza kuiandikia bao timu yake kufuatia mpira uliotemwa na Kipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohamed wakati akiokoa hatari ya Robert Ndaki.

Mtibwa licha ya kupambana kusaka bao la kusawazisha, lakini uimara wa beki na Kipa wa Mbao, Rahim Sheikh haukuwaruhusu 'Wakata Miwa' hao kufanya lolote.

Advertisement

Hata hivyo licha ya matokeo hayo mazuri timu hiyo ya jijini hapa inafikisha pointi 35 na kubaki nafasi yake ya 19, huku Mtibwa Sugar akibaki na alama zake 38 nafasi ya 16.

Advertisement