Mbao yaahidi kubaki Ligi Kuu

Muktasari:

 

Mbao FC inayonolewa na Kocha Abdulmutik Haji, inashika nafasi ya 19 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 23

WINGA wa Mbao FC,Herbert Lukindo amesema wale wote wanaowabeza kuwa watashuka daraja watakata ngebe baada ya msimu huu wa ligi kuu kufikia ukingoni.

Mbao FC yenye maskani yake  jijini Mwanza hadi sasa imeshacheza mechi 28 na wako nafasi ya 19 katika msimamo wa ligi kuu wakiwa na pointi 23.

Timu hiyo ilipanda rasmi ligi kuu msimu wa 2016/17 baada ya maamuzi ya kamati ya nidhamu ya TFF ya kufuta matokeo ya timu za Geita Gold,Polisi Tabora,JKT Kanembwa,JKT Oljoro zilizokumbwa na mkasa wa upangaji matokeo hivyo Mbao kupata nafasi hiyo.

Kufanya vibaya kwa timu hiyo msimu huu kumewafanya wadau wa soka jijini Mwanza kuipa nafasi finyu klabu hiyo ya wauza Mbao kuweza kukwepa janga la kushuka daraja ambapo sasa wamebakiza mechi tisa ili kujiokoa na janga hilo.

Akizungumza na Mwanaspoti Online, Lukindo(20)ambaye msimu huu ni wa tatu kwake akiwa Mbao alisema ili kuwafunga mdomo wale wanaowaponda kuwa watashuka daraja ni muhimu kwao kukomaa na kupata matokeo mazuri kwenye mechi hizo zilizobaki.

Alisema bado nafasi kubwa wanayo ya kupambana na kubaki ligi kuu msimu ujao ambapo amewataka mashabiki wasikate tamaa na maneno ya watu wanaowaponda kuwa wanashuka daraja,

“Nafasi bado tunayo watu wameshatukatia tamaa ya kubaki msimu ujao hii si jambo nzuri mchezo wa soka ni wa maajabu sana tumebakiza michezo 10 ambayo kama tukishinda Sita tu tumebaki kikubwa tutapambana kuhakikisha tunawazima wale wanaotubeza,” alisema Lukindo ambaye pia alishawahi kukipiga Mgambo Shooting na Ndanda.

Alisema ameshacheza mechi 17 za ligi kuu ambapo ameweza kufunga mabao wawili pekee mpaka sasa kitu ambacho amekiri wazi alijiwekea malengo ya kufunga 12 lakini atapambana kuhakikisha michezo tisa iliyobaki angalau anafunga bao tano.