Mbao hakuna kulala, ni matizi mwanzo mwisho

Muktasari:

Hajji alisema kutokana na ushindani uliopo pamoja na malengo yao msimu huu, wameona kutopumzika ni vyema badala yake kipindi hiki wakitumie kurekebisha kasoro zilizojitokeza ili ligi itakapoendelea wawe fiti.

MBAO FC haitaki kupoteza muda katika Ligi Kuu Bara kufuatia kikosi hicho kuendelea kujifua, huku kocha wake msaidizi, Abdul Mutiki Hajji akieleza sababu za kutowapumzisha nyota wao.

Timu hiyo ambayo imecheza mechi 11, imekusanya pointi 14 na kukaa katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ambapo inapambana kukwepa rungu la kushuka daraja.

Kwa sasa ligi hiyo imesimama kupisha kalenda ya michuano ya kimataifa inayotambuliwa na Shirikisho la Soka duniani (Fifa), ambapo Mbao FC wanatumia muda huo kujiweka sawa.

Hajji alisema kutokana na ushindani uliopo pamoja na malengo yao msimu huu, wameona kutopumzika ni vyema badala yake kipindi hiki wakitumie kurekebisha kasoro zilizojitokeza ili ligi itakapoendelea wawe fiti.

Alisema ishu ya timu hiyo kuendelea kunusurika dakika za mwisho kila msimu hawataki ijirudie wakilenga zaidi kumaliza ligi katika nafasi nzuri na kwamba anaamini watafanikiwa.

“Hakuna kulala, ligi ni ngumu, lazima kipindi hiki tukitumie vyema kurekebisha kasoro zilizojitokeza ili michuano ikiendelea tuwe vizuri, hatutaki msimu huu kusubiri matokeo ya mechi ya mwisho” alisema Hajji.

Kocha huyo alisema kwa sasa maeneo anayopambana nayo kuhakikisha yanakuwa imara ni ushambuliaji, beki na kiungo na kwamba, wanahitaji kila mechi kupata ushindi ili wakae katika nafasi nzuri.

“Mwenendo siyo mbaya sana kwa sababu nafasi tuliyopo inatupa nguvu kuendelea kupambana kusaka matokeo mazuri katika mechi zilizobaki, uwezo vijana wanao ili kupata tunachohitaji,” alisema kocha huyo.