Mbao bado sio shwari

KICHAPO cha bao 1-0 ilichokipokea Mbao FC kutoka kwa Kitayosce mwishoni mwa wiki iliyopita kumbe nyuma ya pazia kuna jambo linalosababisha matokeo mabovu.

Mbao ilitua Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi saa chache kabla ya mchezo kuanza na kujikuta ikilala kwa bao hilo lililofungwa na Omari Issa katika dakika ya nane ya mchezo.

Kocha wa timu hiyo, Almasi Moshi mara baada ya mchezo huo alisema jeshi lake bado haliko sawa kutokana na ukata unaozidi kuwatembelea.

“Tuliondoka Mwanza saa tatu asubuhi na tulipofika hatukupata muda mrefu wa kupumzika, nadhani hata kufungwa kumekuwa ni kutokana na makosa tuliyoyafanya,” alisema.

Alisema bado uchumi kwao imekuwa tatizo, suala ambalo hata msimu uliopita lilichangia sehemu kubwa timu hiyo kushuka na nyota wengi kuondoka baada ya msimu kumalizika. Mbao iliwekwa sokoni msimu uliopita baada ya uongozi kushindwa kuwa na uhakika wa kuendelea kuhudumia timu huku wachezaji wakiwa wanadai stahiki zao na kufanya timu kupata matokeo mabovu.

Hadi sasa Mbao imeshuka dimbani maa mbili na kupoteza michezo yote, ilianza kulala 2-1 mbele ya Rhino Rangers na inakamata nafasi ya nane kwenye msimamo wa kundi B.