Mbao FC ya Stam yagawa dozi kinoma

Mwanza. Mbao FC inaendelea kutesti mitambo yake,huku ikiacha gumzo kwa timu inazokutana nazo kwa kuzitembezea vichapo baada ya kuilalua Biashara United mabao 2-1 katika mchezo wa kirafiki uliopigwa mkoani Mara.
Mechi hiyo ya kujipima nguvu kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu kwa Mbao, ilikuwa ya pili baada ya kufanya kweli dhidi ya Masumbwe Warrior kwa kuinyuka bao 1-0 wiki iliyopita.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Masondore Mugango, Biashara United  ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya tisa kupitia kwa Dany Manyenye.
Mbao walitulia na kulisakama zaidi lango la wapinzani wake na kufanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Said Said na kusababisha timu hizo kwenda mapumziko kwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili Mbao ilitawala mchezo huo tofauti na kipindi cha kwanza na kufanikiwa kuongeza bao la pili kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Said dakika ya 50.
Meneja wa Biashara United, Aman Josiah alisema mchezo huo uliwapa mwanga kutambua uwezo wa wachezaji wake na kwamba wao hawakulenga kupata matokeo.
“Mechi hii ilikuwa muhimu kutokana na timu tuliyokutana nayo kiushindani na kwamba licha ya vijana kuonekana kuwa fiti, lakini bado wanahitaji maboresho zaidi,”alisema Josiah.
Kocha wa Mbao, Amri Said ‘Stam’ alisema leo nimeona kuwapo kwa mapungufu kadhaa haswa eneo la ushambuliaji na sehemu ya beki ya kati,lakini matarajio yangu ni kabla ya Ligi kuanza nitakuwa nimeyafanyia kazi.