Mbao FC wanatia huruma

Wednesday March 25 2020

Mbao FC wanatia huruma,Mbao FC inauzwa,mwanasport,ligi kuu Tanzania Bara,Mwanaspoti,

 

By Clezencia Tryphone

TAFSIRI rahisi unayoweza kuitumia kuwaelezea Mbao FC ni kwamba wanatia huruma. Kiuhalisia kwa mujibu wa maelezo ya uongozi ni kwamba, hali ni ngumu ndani na nje ya uwanja.

Uongozi umesisitiza kwamba utahakikisha unapambana timu hiyo ibaki Ligi Kuu Bara licha ya kuwa na madeni lukuki yanayotaka kuwatoa kwenye reli. Mwenyekiti wa timu hiyo, Zephania Njashi anasema wanapambana kwa kila namna ili wafanikiwe katika mambo yote. Mbao FC ni moja ya timu zilizokuwa na ushindani mkubwa kwenye ligi hasa pale zinapokutana na vigogo wa soka Simba na Yanga, kwa sasa inashika nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi 28.

Timu hiyo imeshinda mechi tano ikitoka sare mechi saba na kupoteza mechi 16, msimu huu, ikiwa imeshindwa kufurukuta tofauti na misimu iliyopita.

KUINUSURU

Njashi anasema wanapambana kuhakikisha walau ibakie Ligi Kuu kwani ikishuka daraja ni kazi kubwa kuipandisha kutokana na ushindani uliopo kwenye ligi hiyo.

Anasema kwa sasa wanawaomba wadau wajitokeze kuwasapoti kwa namna yoyote ile kuinusuru Mbao FC, halafu hapo baadaye watajua namna gani ya kufanya kwa kuwa timu hiyo inahudumiwa na watu wachache tofauti na inavyodhaniwa na watu wengi.

Advertisement

“Hivi sasa hatuna kabisa nguvu za kupambana na timu, tunahitaji sana sapoti kutoka nje ili kuinusuru isishuke daraja, ni wakati wa wadau sasa kutushika mkono hii timu iendelee kuitangaza Kanda ya Ziwa,” anasema.

“Kusema ukweli hii timu toka ianze tuko watu 18 ambao tunajitolea pesa zetu wenyewe kwa kushirikiana na wadhamini tulionao kama GF Track kuiendesha.”

Njashi anaongeza kuwa licha ya kuwa na wafanyabiashara wengi jijini Mwanza na mikoa mingine jirani, lakini hawana msaada wa aina yoyote katika timu hiyo. “Hata hapa Mwanza wapo wengi tu, lakini likija jambo la kutoa pesa siyo mchezo, wao kutokana na jina la timu tuliwasogeza kupata walau mashabiki wa kwenda uwanjani kuisapoti timu, wao watachangia kulipa vigoma vya kuhamasisha ila kusema wachangie ndani ya timu hakuna kitu kama hicho,” anasema.

Mwenyekiti huyo anaongeza kuwa kipindi cha nyuma hali ya kiuchumi ilikuwa angalau na hawakuthubutu kujitolea kwa timu tofauti na hivi sasa uchumi umekuwa mgumu.

MADENI LUKUKI

Bajeti ya Mbao FC kwa msimu mzima kuanzia usajili, posho mpaka mishahara ni Sh800 milioni ambayo inaifanya timu kuwa katika kiwango bora kabisa cha ushindani.

Lakini ikishindikana hali yao ikiwa mbaya zaidi piga ua lazima iwe kati ya Sh450 milioni mpaka 500 ambazo ni pesa nyingi na hasa ikizingatia timu haina wadhamini wengi kama zilivyo Simba na Yanga. “Kuendesha timu si mchezo, badala ya kuingiza tunatoa na kubaki na madeni, tunajikuna tunaumia hadi ndani ya uchumi wetu, hili jambo linaumiza, mpira ni burudani sasa unataka kuwa karaha ya kutufanya kuwa na mawazo kila uchao.” Anasisitiza kuwa mpaka sasa wachezaji wao wanawadai mishahara ya miezi mitatu ambayo inamfanya mchezaji kukosa hata morali awapo uwanjani, ila wanapigana kuona namna gani watainusuru timu hiyo yenye jina kubwa hivi sasa.

Njashi anasema timu ikiwa jijini Mwanza hutumia Sh300,000 hadi 400,000 ila ikiwa nje ya mji huo hutumia Sh700,000 hadi 800,000 kwa siku pesa ambazo wao wenyewe hujitolea.

KUTAKA KUIUZA

Anasema kwa sasa timu hiyo haijawekwa sokoni, bado wanapambana kwa kushirikiana na wadau kuinusuru na endapo wakiona maji yamewafika shingoni wataiweka sokoni ili wapate pesa za kulipa madeni ambayo wanadaiwa ili waachane na mpira wafanye mambo mengine.

“Tunapambana kwanza ibaki Ligi Kuu hata tukisema tunaiweka sokoni mnunuzi naye anajua yuko Ligi Kuu na siyo kwingine, tukifeli kupata pesa za kulipa madeni ni kweli tutauza tu tulipe kwani dawa ya deni kulipa,” anasema huku akiwashukuru GF Track kwa udhamini wao ambao umewafikisha hapo walipo.

PONGEZI MWANASPOTI

Njashi analipongeza gazeti hili kwa kuiweka karibu timu hiyo. “Mwanaspoti nawapongeza mmeona mnitafute mimi mtu sahihi ambaye naweza kuzungumzia timu kwani najua uchungu wake kutokana na pesa tunazotoa na wenzangu,” anasema.

Advertisement