Mbao FC sasa yanogewa, akili zote zahamia simba

Tuesday September 11 2018

By SADDAM SADICK

BAADA ya Mbao FC kufanikiwa kuvuna pointi saba ugenini, Kocha wa timu hiyo, Amri Said ‘Stam’ amesema kwa sasa nguvu zote ni katika mechi za nyumbani akianza na JKT Tanzania kuhakikisha hapotezi kitu.

Mbao ambao kwa sasa inaongoza Ligi Kuu kwa pointi saba, itaikaribisha JKT Tanzania mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kirumba, jijini Mwanza Jumamosi hii kabla ya kuikaribisha tena Simba na Prisons baadaye.

Kocha Said alisema kwa sasa wanaendelea kujiwinda vikali kuhakikisha wanavuna kwanza pointi 10 kabla ya kuwavaa watetezi Simba, Septemba 20.

“Mipango yetu kwanza ni kushinda mechi ijayo dhidi ya JKT Tanzania ili tufikishe alama 10 kabla ya kuisubiri Simba na tutakuwa na nguvu zaidi na morali, tunaendelea kujiandaa vyema,” alisema kocha huyo.

Aliongeza maandalizi yao yanalenga kupambana na mechi zote bila kujali ugenini wala ukubwa wa timu, hivyo kila mpambano kwao wanauona kama fainali.

Alisema kikubwa anahitaji Mbao kuondokana na changamoto ya kusubiri matokeo ya kujinasua na janga la kushuka daraja dakika za mwisho, hivyo mashabiki wazidi kuisapoti timu yao.

“Tunajiandaa na kila mchezo bila kujali ukubwa au udogo sijui cha ugenini na nyumbani, kila mechi tunaiona kama fainali kwa hiyo tunataka kuondokana na kusubiri matokeo ya mwisho kushuka daraja,” alisema.

Advertisement