Mbao FC kufyeka na kuongeza wanne

Muktasari:

Mbao imekusanya pointi 17 na kukaa nafasi ya 11 baada ya kushuka uwanjani mara 13 ambapo inarudi kambini baada ya mapumziko mafupi kuendelea na mazoezi.

WAKATI Mbao FC ikitarajia kurudi kambini leo Ijumaa, benchi la ufundi limesema kwa sasa linasubiri kipyenga cha dirisha dogo la usajili ili kupunguza na kuongeza nyota wanne.

Usajili huo unatarajiwa kufunguliwa Disemba 15 mwaka huu ambapo timu hiyo imepanga kuongeza nguvu kikosini ili kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Mbao imekusanya pointi 17 na kukaa nafasi ya 11 baada ya kushuka uwanjani mara 13 ambapo inarudi kambini baada ya mapumziko mafupi kuendelea na mazoezi.

Kocha Msaidizi wa Mbao FC, Abdulmutiki Hajji alisema katika kuhakikisha wanarejea kwa kasi uwanjani, wanatarajia kufyeka wachezaji wanne na kuongeza idadi hiyohiyo.

Alisema nafasi watakazoongezea nguvu ni beki wa kati, kiungo mkabaji na washambuliaji wawili ambao watakuwa na uwezo wa kubadili upepo kikosini na kuiletea ushindi timu.

“Lazima tuache na kuongeza wanne, tumeona mapungufu nafasi za beki wa kati, kiungo na straika kwahiyo ili kuweza kuendana na hali na mabadiliko tunapaswa kufanya hivyo”alisema Hajji.

Kocha huyo aliongeza kuwa licha ya kwamba hawajawa na mwenendo mbaya sana, lakini wanaamini watakapoanza mazoezi watarekebisha kasoro zilizopo ili mechi zinazofuata ikiwamo michuano ya FA wafanye kweli.

“Tunatarajia kuingia kambini Ijumaa (leo) kujiandaa na Ligi Kuu lakini tuna mchezo wa Kombe la Shirikisho, kwahiyo tutafanyia kazi mapungufu ili kupata matokeo mazuri," alisema