Mbao FC haitanii kuzibana Simba, Yanga SportPesa Cup

Muktasari:

  • Michuano ya Sport Pesa inatarajia kuanza Januari 22-27 mwakani,ambapo timu za Simba,Yanga,Singida na Mbao(Tanzania),Gor Mahia,Bandari,AFC Leopard na Kariobangi Sharks kutoka Kenya.

 

 KLABU ya Mbao FC imesema kuwa itatumia vyema fursa ya kushiriki michuano ya Sports Pesa kuhakikisha inaonyesha ushindani mkali na kuweza kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Mbao ya Jijini hapa ilifanikiwa kuwa miongoni mwa Klabu shiriki kwenye michuano hiyo kama timu mwalikwa inayoshirikisha timu nane kutoka Tanzania na Kenya.

Kocha wa Mkuu wa timu hiyo, Amri Said ‘Stam’ alisema kuwa hiyo ni fursa kwao muhimu kuhakikisha wanaitumia vyema katika kujitangaza kimataifa kupitia michuano hiyo.

Alisema kuwa hatarajii Ligi Kuu kuweza kuwaharibia mipango kutokana na kikosi chake kuwa kipana na chenye ushindani hivyo wanaona ni nafasi nzuri kwao kuonyesha uwezo kwenye soka.

“Ni fursa kubwa kwetu kuonyesha ubora wetu,sidhani kama Ligi Kuu itaathiri chochote kwa sababu kikosi changu ni kipana na vijana wana uwezo kwenye soka,lazima tutwae Ubingwa na kujitangaza kimataiafa”alisema Stam.

Kocha huyo bora wa Ligi Kuu mwezi Agosti,alisema kuwa kwenye michuano hiyo Mbao inawakilisha Mikoa ya Kanda ya Ziwa,hivyo lazima ifanye kweli ili kuweka rekodi mpya kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo.

Alisema kuwa wadau na mashabiki wa soka ndani na nje ya Mkoa wa Mwanza wasubiri kuona burudani kwani Mbao ni timu yenye ushindani bila kujali aina ya Ligi.

“Mbao inawakilisha Mwanza lakini hata mikoa ya Kanda ya Ziwa wanatutegemea kwahiyo lazima tupambane kuwakilisha vyema,niwaombe wadau na mashabiki kutusapoti na sisi tumejipanga kuwapa furaha”alisema Kocha huyo.