Mbangula Shujaa wa Prisons aliyeizamisha Simba

MASHABIKI wa Simba hawana hamu hata kidogo na Tanzania Prisons. Ni timu ambayo kwa misimu kadhaa imekuwa ikiwasumbua na juzi kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu, iliwaliza kwa kuwatungua bao 1-0.

Bao hilo pekee la dakika ya 49 lilitibua rekodi waliyokuwa nayo ya kucheza mechi 10 mfululizo za mashindano kwa muda wa siku 98 ambazo ni sawa na saa 2, 352 bila kuonja kipigo chochote.

Zile kelele la Simba pira biriani...pira pishori na kelele nyingine za mashabiki wa Simba zilizimwa na pira gwaride kupitia mpira wa kichwa uliopigwa kiufundi na mshambuliaji Samson Mbangula mbele ya beki kisiki, Joash Onyango na kumuachia msala kipa Aishi Manula.

Kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, Simba ilionekana kupoteza soka lake tamu, pengine kutokana na kukosekana kwa nyota wake kadhaa ikiwamo injini yao, Clatous Chama na mitambo ya mabao - Meddie Kagere, John Bocco na Chris Mugalu.

Alichokifanya Mbangula kimeipa jeuri Prisons kumaliza ukame wa misimu minne bila kushinda mbele ya Wekundu wa Msimbazi. Mara ya mwisho Prisons kuifunga Simba ilikuwa msimu wa 2016-2007 walipoifumua nyumbani mabao 2-1 kipindi hicho ikicheza jijini Mbeya.

MSIKIE MBANGULA

Bao la juzi dhidi ya Simba lilikuwa la kwanza kufungwa na Mbangula msimu huu na kuipa timu yake pointi tatu zilizoifanya ifikishe alama tisa baada ya mechi saba na mfungaji huyo anasema: “Kila mchezaji, hususan mshambuliaji anajisikia vizuri kufunga katika mechi ili kuipa matokeo timu yake, nami najisikia furaha na faraja.”

Anasema alichokifanya wakati beki wake wa kulia, Michael Ismail akiupiga mpira mrefu baada ya kurushiwa na Salum Kimenya, alitafuta mbinu ya kuwazidi ujanja mabeki wa Simba.

Mbangula anasema licha ya Onyango kuwa mrefu zaidi yake alichokifanya ni kuangalia nafasi ya mpira na ‘timing’ ndicho kilichomfanya kuwahi kuruka na kuizidi ujanja safu ya Simba na kufunga mpira kwa kichwa.

“Kwa kweli niliuangalia mpira ulipokuwa unakuja nikamzidi ujanja Onyango kwa kuruka zaidi yake na kutumbukiza nyavuni, pia nilishamuona Manula ametoka langoni,” anasema Mbangula na kuongeza:

“Nimefarijika sana, lakini bado nawaomba mashabiki wa Prisons waendelee kuisapoti timu yao bila kuchoka, kwani kuanza kwetu vibaya kwenye ligi ni mambo ya kiufundi zaidi, lakini kila kitu kitakaa sawa, bado tuna mechi 27 mbele kabla ya kumaliza msimu, lakini tupambane.”

KUMBE BEKI BUANA

Mshambuliaji huyo aliyemaliza na mabao manane msimu uliopita, alianza soka tangu akiwa shule ya msingi, lakini alifahamika zaidi akiwa masomoni katika Sekondari ya Isoho iliyopo Mbeya.

Anasema nyota yake kisoka ilianza kung’ara akiwa kidato cha tatu hadi nne akiichezea Airport Rangers ya Ligi Daraja la Tatu ,na baada ya kumaliza shule alitimkia Kigoma kwa ajili ya shughuli nyingine za kiserikali.

Mbangula ambaye ni askari Magereza, anasema baada ya kutoka Kigoma alitua Magereza Dar FC ya jijini Dar es Salaam mwaka 2017 na kudumu hapo hadi msimu wa 2018/19 alipoiwezesha kupanda Ligi Daraja la Pili (SDL) na tangu awali alikuwa akicheza kama beki wa kati.

“Kwa muda wote huo nilikuwa nacheza nafasi ya beki wa kati, lakini kocha wangu, Oraph Mwamlima akaamua kunibadilisha namba kutokana na nilivyokuwa nacheza. Sifahamu alikiona nini kutoka kwangu na hajawahi kuniambia kwa nini alinibadili namba,” anasema.

Mbangula anasema baada ya kuhamishwa namba kikosini alizidi kufanya vizuri zaidi na anakumbuka alimaliza msimu kwa kufunga mabao 19 wakati akiwa na timu hiyo ya Ligi Daraja la Tatu.

MAKALI YA ADOLPH

Mbangula anasema kwa msimu uliopita makali yake yaliongezeka alipojiunga na Prisons baada ya kujazwa upepo zaidi na Kocha Mohammed Rishard ‘Adolph’.

Anasema alijituma na kumshawishi Adolph ambaye kwa sasa hayupo Prisons kumpa nafasi na kufunga mabao muhimu yaliyoisaidia timu yao kwenye mikikimikiki ya Ligi kuu iliyopita. “Pia kuna mengi ya kujifunza kwa wachezaji wenzangu, uongozi na benchi la ufundi kwa jinsi wanavyonisapoti na kunitia nguvu kwenye kazi hii hadi hapa nilipofika, nidhamu ndio kila kitu kwenye soka na yote ni kwa sababu ya msingi wanaonipa wao.”