Mbangula Kutoka beki kitasa hadi mshambuliaji tegemeo

Muktasari:

Alianza soka katika Shule ya Sekondari ya Isoho iliyopo Mbeya, na akiwa kidato cha tatu hadi nne wakati alikipiga Airport Rangers ya Ligi Daraja la Tatu na baada ya kumaliza shule alitimkia Kigoma kwa ajili ya shughuli nyingine za kiserikali.

ULE msemo kwamba kipaji hakijifichi wale waliousema hawakukosea kusema hivyo, kwani tumeona vijana wengi ambao wanakipiga na kuonyesha uwezo wao kila wanapopata nafasi ya kuingia uwanjani hata kama ni dakika chache.

Ndani ya ‘Wajelajela’, Tanzania Prisons sio tu wanatamba na rekodi ya kutofungwa mchezo hata mmoja kwenye Ligi Kuu mpaka sasa, pia kuna dogo anakuja juu kwa kasi ya kutisha. Huyu ni Samson Baraka Mbangula aliyeweka kambani mabao manne katika Ligi Kuu Bara.

Alianza soka katika Shule ya Sekondari ya Isoho iliyopo Mbeya, na akiwa kidato cha tatu hadi nne wakati alikipiga Airport Rangers ya Ligi Daraja la Tatu na baada ya kumaliza shule alitimkia Kigoma kwa ajili ya shughuli nyingine za kiserikali.

Mbangula (24), ambaye ni askari kwenye kikosi cha Tanzania Prisons, anasema baada ya kutoka Kigoma alitua Magereza Dar FC ya Dar es Salaam mwaka 2017 na kudumu hapo hadi msimu uliopita walipoiwezesha kupanda Ligi Daraja la Pili (SDL).

“Kwa muda wote huo nilikuwa nacheza nafasi ya beki wa kati, lakini kocha wangu Oraph Mwamlima aliamua kunibadilisha namba kutokana na nilivyokuwa nacheza,” anasema.

“Sifahamu alikiona nini kutoka kwangu na hajawahi kuniambia kwa nini alinibadili namba, lakini baada ya kuhamishwa namba nilizidi kufanya vizuri zaidi, nilimaliza msimu uliopita nikiwa na mabao tisa na wakati timu ikiwa Ligi Daraja la Tatu nilifunga mabao 19.”

Kutokana na kasi yake ndani ya dimba, msimu huu alisajiliwa Tanzania Prisons na huko anazidi kumshawishi Kocha Mohammed Rishard ‘Adolf’ kwamba hakukosea kumsajili na sasa amemiliki namba ndani ya kikosi.

“Kuna mengi ya kujifunza kwa wachezaji wenzangu, uongozi na benchi la ufundi kwa jinsi wanavyonisapoti na kunitia nguvu kwenye kazi hii hadi hapa nilipofika, nidhamu ndio kila kitu kwenye soka na yote ni kwa sababu ya msingi wanaonipa wao,” anasema.

Msimu huu bao lake la kwanza alifunga wakati wakiifunga Mtibwa mabao 3-1 huku mengine yakifungwa na Benjamin Asukile na Jeremiah Kisubi na lile la kufutia machozi la Mtibwa likifungwa na Isa Kajia Kigingi.

Bao la pili alifunga kwenye sare ya bao 1-1 mbele ya Alliance kisha akatupia walipokabana koo ya bao 1-1 na Mbao FC na la nne akafunga kwenye sare ya bao 1-1 pia mbele ya Mwadui FC.