Mazoezi ya Mkongo Yanga tema mate chini

Morogoro. Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera ameendelea kuiongezea makali timu yake katika kumalizia mechi za Mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu Bara lakini mambo matatu ameonekaa kuyawekea mkazo mkubwa katika kambi yao.
Pumzi ya kutosha
Akimaliza siku ya 11 leo akiwa na kikosi chake kambini Mkoani Morogoro Zahera ameonekana kutilia mkazo mkubwa pumzi ya wachezaji wake katika maandalizi hayo.
Wakiwa hapa Zahera amekuwa kila baada ya siku mbili anarudisha dozi ya mazoezi ya pumzi ambapo mazoezi hayo yamekuwa yakifanyika kwa mbio zenye njia tofauti.
Kocha huyo raia wa DR Congo amekuwa akiwakimbiza wachezaji wake kwa mbio za kasi kubwa akitaka kuona ndani ya sekunde tano vijana wake wanafika katika kituo kimoja huku wakati mwingine akiwataka kukimbia kwa kuchezea mpira.
Zoezi hilo linaonekana kuwapa uhai wachezaji wake ambapo katika mchezo wa juzi dhidi ya timu ya Morogoro Tanzanite Academy licha ya ushindi walioupata wa mabao 5-1 Yanga ilionekana kuwa imara kwa pumzi ikiwasadia kutengeneza mashambulizi na kukaba kwa haraka.
Stamina
Wachezaji wa Yanga sasa wanaonekana kuwa imara kwa nguvu ya mwili ambapo sio rahisi kuweza kuwapokonya mipira wanapombana kwa mwili.
Mkongomani huyo amekuwa akiwafanyisha mazoezi makali ya kuongeza nguvu ambapo jana aliwataka wachezaji wake kugawana wawili wawili huku mmoja akimshika miguu mwenzake kwa nyuma na aliyeshikwa kutembea kwa mikono kwa dakika moja na nusu.
Zoezi hilo liliwapa wakati mgumu wachezaji wengi ambapo kocha huyo alionekana kuwa makini akiwataka kila mmoja kufanya kwa kiwango anachokitaka.
Ufundi pia upo
Katika mazoezi ya jioni Zahera amekuwa akiwabadilishia dozi wachezaji wake akihamia katika mazoezi ya ufundi wa uwanjani ambapo huko amekuwa akiwapa mbinu mbalimbali za uwanjani.
Kocha huyo amekuwa akitoa maelekezo kwa kila idara uwanjani na majukumu yake katika kuanzisha mashambulizi kuanzia kwa mabeki wanafuata viungo na mpaka kwa washambuliaji na namna ya kufunga.
Katika eneo hilo kocha huyo amekuwa kila wakati anasimamisha mpira na kutoa maelekezo kwa kuwasahihisha anapoona wanakosea kile anachokitaka wakifanye.
Akiwa na viungo ameonekana kutaka kuona kila kiungo akihusika katika kutengeneza mashambulizi sambamba na kukaba huku akikataza kabisa kuona mchezaji wa eneo hilo akitembea au kukimbia taratibu.
Washambuliaji nao amekuwa akisisitiza utulivu katika kumalizia huku akitaka kuona mashuti makali yanahusika kama njia ya kupata mabao.