Mayweather arejea ulingoni kucheza Kickboxing

Muktasari:

Pambano hilo la mchanganyiko wa ngumi na mateke ‘Kickboxing’ litachezwa usiku wa mkesha wa mwaka mpya Desemba 31

Los Angeles, Marekani. Bondia Floyd Mayweather ameamua kurejea ulingoni kwa kusaini mkataba wa kupanda ulingoni kucheza kinda anayetisha katika kickboxing, Tenshin Nasukawa wa Japan.

Pambano hilo la mchanganyiko wa ngumi na mateke ‘Kickboxing’ litachezwa usiku wa mkesha wa mwaka mpya Desemba 31 ikiwa ni maalumu kuuaga mwaka 2018 na kuukaribisha 2019, nchini Japan.

Uamuzi huo umewastusha wadau wengi wa ngumi hasa ikizingatiwa bondia huyo aliyestaafu ngumi na ambaye hajawahi kushindwa tangu amejitosa katika ngumi za kulipwa akishinda mapambano yake yote 50 alitarajiwa kurudiana na Manny Pacquiao wa Ufilipino.

Wawili hao walipanda ulingoni mwaka juzi katika pambano lililoandika rekodi kutokana na kuingiza fedha nyingi na ushindi wa Mayweather ulipingwa na kambi ya Pacquiao na alikubali kurudiana naye.

Bingwa huyo mara 50 wa Dunia alitangaza kustaafu kabla ya kurejea ulingoni Agosti mwaka jana na kumshinda Conor McGregor katika pambano lake la 50.

“Ninataka kufanya kitu tofauti, ninatamani kufanya hivyo nje ya Marekani, ninataka kuwapa watu kile waanchokipenda ambacho ni machozi, jasho na damu,” alisema. 

Mayweather kambi yake na mpinzani wake zipo katika mazungumzo kuamua kanuni zitakazotumika katika mchezo huo.

Nasukawa, mwenye miaka 20, anayewakilishwa na RIZIN Fighting Federation, ni bingwa anayetambuliwa na Chama cha Kickboxing ameshinda mapambano yake yote 27 aliyocheza.