Mayanga wala hana presha Ruvu Shooting

Muktasari:

Mayanga amechukua mikoba ya kuinoa timu hiyo mwishoni mwa mwezi uliopita kutoka kwa Abdulmutic Haji aliyetimkia Mbao FC.

KOCHA Mkuu wa Ruvu Shooting, Salum Mayanga amesema licha ya kuchelewa kuanza kwa mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kwa timu yake, haimtii hofu yoyote kwani atatumia wiki mbili zilizobaki kupanga silaha za maangamizi.

Mayanga amechukua mikoba ya kuinoa timu hiyo mwishoni mwa mwezi uliopita kutoka kwa Abdulmutic Haji aliyetimkia Mbao FC.

Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar amekiri ligi ya msimu ujao itakuwa sio ya kitoto kwani timu zimeonekanaa hazitaki utani kwa kusajili wachezaji wa maana,” alisema.

“Hivi sasa nakimbizana na muda kwani tulichelewa sana kuanza mazoezi, hivyo naamini baada ya wiki mbili tutakuwa tuko vizuri tayari kwa ligi.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya kwenye ligi na muhimu zaidi ni kuanza ligi vizuri na kujipanga mwanzo kabisa ili huko mbele mambo yasiwe magumu zaidi.

“Kama unavyojua msimu ujao timu zinazoshuka daraja ni nyingi, hivyo lazima tukomae tusiwe miongoni mwao ndio maana tunatakiwa kuanza kupiga hesabu zetu vizuri tangu mwanzo wa msimu.”

Msimu wa 2020/2021 timu za Ligi Kuu Bara zitakuwa 16 badala ya 20 baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kubaini kuwepo kwa changamoto kubwa msimu uliopita kutokana na kukosekana kwa mdhamini wa ligi.