Mayanga awataka viongozi Mbao kujipanga

Muktasari:

  • Mayanga alikuwa Kocha wa tatu kuinoa Mbao baada ya watangulizi wake,Amri Said na Ally Bushiri kushindwa kuendelea nayo kwa sababu tofauti.

MBAO FC imenusurika kushuka daraja msimu ambao kocha wao Salum Mayanga ametoa ushauri kwa mabosi wake ambao wakiuzingatia na kuufuata watafanya vizuri.
Mayanga amewataka viongozi wa Mbao kufanya maandalizi mapema ikiwemo kusajili kikosi chenye ushindani kwa kile alichoeleza kwamba ligi ya sasa imekuwa ngumu.
Amesema ili kuepuka kutafuta pointi za kubaki kwenye ligi, ni vyema hayo mambo yakafanyika mapema kwani kuinusuru timu dakika za mwisho sio kazi rahisi.
Mbao imeshiriki Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu sasa ambapo msimu uliomalizika ilikuwa na matokeo mabaya na kujikuta ikisubiri mechi ya mwisho kujihakikishia kubaki msimu ujao.
Mayanga ambaye alikuwa kocha wa tatu kuifundisha timu hiyo ndani ya msimu mmoja aliikuta Mbao ipo nafasi mbaya na kuanza kupambana kuibakisha kwenye ligi.
Mbao ilinowa na makocha Amri Said ‘Stam’ ambaye alitimkia Biashara United, kisha nafasi yake ilichukuliwa na Ally Bushiri ambaye alitupiwa virago na kurithiwa na Mayanga.
Mayanga aliliambia Mwanaspoti kuwa alipoikuta timu hakuamini kama itanusurika, lakini kujituma kwa vijana na kufuata maelekezo yake ndio ilisaidia.
Alisema ligi ilikuwa ngumu kwa timu nyingi kuonyesha ushindani hadi kubaini timu zitakazoshuka daraja kupatikana mechi za mwisho na kwamba lazima uongozi uzingatie ripoti yake.
“Baada ya wiki mbili hivi nitatoa taarifa rasmi lakini kwa ufupi nimekabidhi ripoti kwa viongozi ambapo nimeshauri mambo ya kufanya kwa ajili ya msimu ujao, ligi ilikuwa ngumu”alisema Mayanga.
Kocha huyo aliongeza kuwa lazima msimu ujao wafanye maandalizi mapema pamoja na kuvuna pointi mechi za mwanzo kuondokana na kusubiri matokeo ya mwisho.