Maxime kupiga moja kisha TPL

Muktasari:

Timu hiyo iliponea tundu la sindano kushuka daraja msimu uliopita.

KAGERA Sugar imesema mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Gipco FC utakaopigwa kesho Jumapili mjini Bukoba ndio utakaohitimisha ratiba ya maandalizi yao na kusubiri Ligi Kuu.

Timu hiyo ya mkoani Kagera hadi sasa imeshacheza mechi tano za kujipima nguvu na kushinda nne ikiwa ni dhidi ya Aigle Noir ya Burundi, Singida United, Prisons na Mwadui FC huku ikitoka sare na Gwambina FC.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime alisema mchezo huo dhidi ya Gipco FC inayojiandaa na Ligi Daraja la Kwanza ndio utakuwa wa mwisho katika kujiandaa na Ligi Kuu inayotarajia kuanza Septemba 23.

Alisema mechi walizocheza za kirafiki zimesaidia kwa kiasi kikubwa kukijenga kikosi chake na kutamba kuwa ligi ikianza Kagera Sugar itazihenyesha timu nyingi. “Tunafunga mechi za kirafiki na Gipco kwa sababu tulihitaji kucheza na KCC, lakini wanajiandaa na mechi za kimataifa kwa hiyo baada ya mchezo huo tutasubiri rasmi Ligi Kuu kuanza,” alisema Maxime.

Kocha huyo alitamba kuwa hadi sasa nyota wake wako fiti na hata ligi ikianza wapo tayari kukiwasha na kwamba, msimu ujao wamedhamiria kufanya kweli.

Aliongeza kuwa kinachompa nguvu ni jinsi vijana wake walivyoonyesha ubora wao kwani katika mechi walizocheza hawakupoteza hata moja, huku wakiruhusu mabao mawili katika nyavu zao. “Siwezi kusema kwamba mabeki ni wazuri kuliko washambuliaji kwa sababu hii ni timu na kila mmoja anashirikiana na mwenzake, kwa hiyo najivunia kwa kikosi chote,” alisema kocha huyo.

Timu hiyo iliponea tundu la sindano kushuka daraja msimu uliopita.