Maxime awaita Yanga mezani

Muktasari:

Maxime aliyewahi kuinoa Mtibwa Sugar, alisema amefungua milango kwa Yanga kama wameridhishwa na kazi yake.

Mwanza. Kocha wa Kagera Sugar Mecky Maxime amesema yuko tayari kujiunga na Yanga endapo klabu hiyo itampa dau analotaka.

Kauli ya Maxime imekuja muda mfupi baada ya kuiongoza Kagera kupata ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, juzi.

Akizungumza jana, Maxime alisema ingawa ana sifa ya kuwa kocha mkuu, lakini kama Yanga wanamtaka atakuwa tayari kuwa msaidizi wa Luc Eymael.

Maxime aliyewahi kuinoa Mtibwa Sugar, alisema amefungua milango kwa Yanga kama wameridhishwa na kazi yake.

“Nina Leseni A ya Caf (Shirikisho la Soka Afrika), Yanga wananihitaji niwe kocha msaidizi sina tatizo mimi naangalia maslahi wakinipa zaidi ya ninachopata Kagera Sugar nitaenda” alisema kocha huyo.

Kocha huyo alisema anaendelea kuheshimu mkataba wake na Kagera na klabu inayomtaka inapaswa kufuata utaratibu.

Pia Maxime aliwapongeza wachezaji kwa kazi nzuri waliyofanya katika mchezo dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.