Maxime alianzisha mapema Bara

Muktasari:

Maxime alisema kikosi chake kitaanza rasmi mazoezi yao kesho Jumatano jijini Dar es Salaam na wataitumia siku ya leo kwa ajili ya kutambulishana na kuwekana sawa.

MAKOCHA Mwinyi Zahera na Patrick Aussems pamoja na wenzao wajipange tu, la sivyo wanaweza kuaibika mbele ya Kagera Sugar ambayo kupitia kocha wake mkuu, Mecky Maxime ametamba kuwa usajili aliofanya vigogo vya soka nchini vijiandae tu kisaikolojia.

Kocha Maxime alisema anaamini kwa usajili alioufanya msimu huu, vigogo hivyo na wapinzani wao wengine lazima wajiandae tu kuumia kwani 2019-2020 ni zamu yao kubeba ndoo.

Kauli ya Maxime imekuja baada ya jana Jumatatu kumsainisha kipa Benedict Tinocco aliyekuwa Mtibwa Sugar, huku akimalizana pia na straika Mganda, Jackson Kibirige.

Kocha huyo ambaye amekuwa akiinyima raha Simba kwa misimu mitatu sasa, alisema kwa aina ya usajili alioufanya anadhani Kagera itakuwa tishio kuliko misimu iliyopita.

“Wengi wanajadili juu ya usajili wetu, kwangu naona ni wa kiwango cha juu na utanipa matokeo mazuri msimu ujao. Sehemu kubwa ni wapya na nimesajili kwa matakwa yangu,” alisema Maxime aliyeingiza sura mpya na kupukutisha wale wa zamani.

Maxime alisema kikosi chake kitaanza rasmi mazoezi yao kesho Jumatano jijini Dar es Salaam na wataitumia siku ya leo kwa ajili ya kutambulishana na kuwekana sawa.

“Tutafanya mazoezi hayo Dar es Salaam kwa wiki moja na baadaye tutahamia Bukoba kwa maandalizi mengine zaidi,” alisema.

Mbali na Tinocco, Maxime aliyekuwa nahodha wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars miaka kadhaa iliyopita kabla ya kustaafu, amewasajili Jackson Kibirige, Abdul Kassim, Said Kipao, Chalamanda, Mwaita Gereza, Ally Shomary, Haroun Kheri na David Luhende.

Wengine ni Juma Shemvuni, Juma Nyosso, Erick Kyaruzi, Hassan Isihaka, Majid Khamis, Zawadi Mauya, Mussa Haji Mosi, Ally Ramadhani na Abdallah Seseme.

Wapo pia kina Peter Mwalyanzi, Japheth Makalayi, Yusuf Mhilu, Geofrey Mwashiuya, Awesu Awesu, Erick Mwaijage, Frank Ikobela, Everist Mujwahuki na Nassor Kapama.