Mawigi wa Ligi Kuu England

Muktasari:

Staili ya nywele imekuwa kitu muhimu kwa wanasoka wa kisasa, lakini hii ndio orodha ya wachezaji wenye nywele kama wamevaa mawigi kwenye Ligi Kuu England.

ACHANA na Paul Pogba, ambaye amekuwa akibadili staili yake ya nywele katika kila mechi. Kuna mastaa hao wa Ligi Kuu England wenyewe wameng'ang'ana na staili moja tu ya mtindo wa nywele ni kuziacha kuonekana kama wamevaa wigi.
Kwenye hilo, hii ndiyo orodha ya mastaa watano matata kwenye Ligi Kuu England ambao staili yao ya nywele kama wamevaa wigi!

5.Mohamed Salah (Liverpool)
Baada ya kuwa na mwanzo mzuri kwenye kikosi cha Liverpool, staa wa Misri, Mohamed Salah amejikusanyia mashabiki kibao kutoka kila pembe ya dunia. Kitu hicho kimemfanya kuwa maarufu kiasi cha kuwafanya hata mashabiki wengine kuanza kufuga nywele zao na kuziacha kuonekana kama afro ili tu wafanane na mkali huyo aliyebeba Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England msimu uliopita. Mo Salah ni mmoja wa mastaa mawigi wanaotamba kwenye Ligi Kuu England kwa sasa.

4.Willian (Chelsea)
Tangu alipotua kwenye Ligi Kuu England huko Stamford Bridge kujiunga na Chelsea akitokea Anzhi mwaka 2013, kiungo wa pembeni wa Kibrazili, Willian amekuwa na mtindo wake uliomfanya kuwa maarufu wa afro. Staa huyo hajawahi kuwa na mwonekano tofauti tangu alipotua kwenye ligi hiyo, akifuga nywele zake kuwa kubwa kama vile amevaa wigi. Wakati mwingine Willian amekuwa akizipiga 'curly' nywele zake ili kuzifanya kuwa na mwonekano huo.

3.David Luiz (Chelsea)
Beki wa Kibrazili anayekipiga huko kwenye kikosi cha Chelsea yenye maskani yake Stamford Bridge, David Luiz amekuwa akiweka nywele zake katika mtindo ambao unapendwa na mashabiki wake. Kwa mujibu wa uchunguzi wa kisayansi ni kwamba wanamichezo wenye nywele nyingi wamekuwa wakiondokana na tatizo la kupata stresi. Hivyo, Luiz amekuwa akiendelea kutumia mtindo wake huo wa nywele ndefu ili kujikinga na stresi.

2.Marouane Fellaini (Man United)
Kiungo wa Manchester United, Marouane Fellaini amekuwa maarufu kwenye Ligi Kuu England kutokana na mtindo wake wa nywele, afro. Mtindo huo wa nywele unaonekana kuendana naye vyema, lakini anakuwa staa mwingine kwenye ligi hiyo mwenye mwonekano kama amevaa wigi kichwani. Kiungo huyo wa zamani wa Everton amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Man United hasa kwa kipindi hiki ikiwa chini ya Jose Mourinho.

1.Matteo Guendouzi (Arsenal)
Mwaka huu, Ligi Kuu England imempata staa mpya anayefanana kwa namna fulani la beki wa Chelsea, David Luiz. Staa huyo mpya anaitwa, Matteo Guendouzi na amejiunga na Arsenal akiwa kiungo wa kati. Mtindo wake wa nywele unaonekana kama wigi unamfanya kiungo Mfaransa huyo kuwa mawigi mwingine aliyekuja kuwashika kwenye Ligi Kuu England. Amekuwa kwenye kiwango bora kabisa akiwa chini ya kocha Unai Emery.