Mawaziri wawili kuongoza Kili marathoni, ulinzi waimarishwa

Muktasari:

Kwa wageni wanaoingia na kutoka kwenye mji huo hata bila kuambiwa watajua nini kinaendelea kutokana na barabara zinazoingia na kutoka kwenye mji huo kupambwa na mabango yanayoashiria uwepo wa mbio hizo kubwa za fedha nchini zinazopewa sapoti na TBL kwa miaka zaidi ya 10.

WAZIRI wa Mali Asili na Utalii, Dk Hamis Kigwangala na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ni miongoni mwa vigogo wa Serikali watakaokimbia kwenye mashindano ya mbio za Kilimanjaro Marathoni.
Mbio hizo zitafanyika keshokutwa Jumapili zikianzia viwanja vya Ushirika mjini Moshi, huku waandaaji wakibainisha kuimarisha ulinzi kwenye barabara zote za mjini hapa ambako wanariadha watapita.
Mjumbe wa kamati ya mbio hizo zinazodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, John Bayo amesema maandalizi yako hatua za mwisho na zoezi la uandikishaji litafungwa kesho Jumamosi saa 6.00 mchana.
Tayari wanariadha mbalimbali kutoka nje ya mji wa Moshi na nchi jirani wako mjini Moshi tayari kwa mbio hizo ambazo kwa mujibu wa Bayo zitaanza saa 12.45 asubuhi kwa marathoni, saa 1.00 asubuhi zile za nusu marathoni na 1.30  zile za kilomita tano.
Mbio zote zitaanzia kwenye uwanja wa Ushirika na kupitia barabara ya Kilimanjaro kuelekea Soweto na kwenda hadi TPC na kurudia njia ambayo wanariadha wa nusu marathoni watapita barabara ya KCMC, Mwika, Masoka, Kilimanjaro na kurudi uwanjani.
"Maandalizi yako kwenye hatua ya mwisho ikiwa ni pamoja na zoezi la uandikishaji ambalo litafungwa saa 6.00 mchana mjini Moshi ambapo tunatarajia hadi usajili unafungwa tuwe na washiriki wasiopungua 20,000," alisema Bayo.
Hadi Alhamisi jioni, wanariadha 6300 walikuwa wamejiandikisha kushiriki.
Alisema Waziri Kigwangala ndiye atakuwa mgeni rasmi sanjari na mwenyeji wake wa Dk Mwakyembe.
Alisema usalama wa wanariadha umeimarishwa katika barabara zote watakazopitia ambapo askari 310 wa usalama barabarani watakuwa barabarani kuhakikisha usalama wakati wa mbio hizo.