Mawakili wa utetezi wakwamisha kesi ya Aveva

Tuesday July 16 2019

 

By Hadija Jumanne

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kuendelea na ushahidi katika kesi ya kughushi na kutakatisha fedha inayowakabili vigogo watatu wa klabu ya Simba kutoka na mawakili wa utetezi kushindwa kufika Mahakamani hapo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa rais wa Simba, Evans Aveva, Makamu wa wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Kesi hiyo imeshindwa kuendelea kutokana na mawakili wa utetezi ambao ni Kung'e Wabeya na Nehemia Nkoko, kuwa katika kesi nyingine iliyopo Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi na Ufisadi, wakati Wakili Benedict Ishabakaki anayemtetea Hanspoppe yeye alipata udhuru, na hivyo kushindwa kufika Mahakamani hapo.

Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai aliimbia mahakama hiyo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya upande wa mashtaka kujibu hoja zilizotolewa na upande wa utetezi.

"Kesi imekuja kwa ajili ya upande mashtaka kujibu hoja zilizowasilisha na upande wa utetezi juu ya kupinga kielelezo kilichowasilishwa mahakamani na upande wa mashtaka tuko tayari kuendelea, lakini mawakili wa utetezi nimeambiwa wanakesi nyingine Mahakama Kuu," alidia Swai na kuongeza

"Kutokana na hali hii, tunaomba Mahakama ipange tarehe nyingine ili tuweze kuendelea na kesi hii" alidia Swai.

Advertisement

Hakimu Simba baada ya kusikiliza Maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 23, 2019 itakapoendelea.

Mshtakiwa Aveva na Nyange wao walirudishwa rumande kutokana na mashtaka ya utakatishaji fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana huku, Hans Poppe akiwa nje kwa dhamana.

Julai 11, 2019 upande wa utetezi kupitia Wakili wao, Nehemia Nkoko, ulipinga maelezo ya onyo aliyotoa Aveva, wakati akiwa polisi yasipokelewe mahakamani hapo kama ushahidi kutokana na kwamba yalichukuliwa kinyume cha sheria.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo ili kutoa nafasi kwa upande wa mashtaka kuja kujibu hoja hizo leo (Julai 16, 2019).

Tayari mashahidi saba wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Miongoni mwa mashahidi hao ni Mchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) Frank Mkilanya(45) ambaye aliieleza mahakama hiyo kuwa viongozi hao wa Klabu ya Simba, , walikiuka maagizo ya yaliyotolewa na Kamati Tendaji ya Klabu hiyo ya kufungua akaunti maalumu kwa ajili ya kutunza fedha, kiasi cha dola za kimarekani 319,212 zilizotokana na uhamisho wa mchezaji wao, Emmanuel Okwi.

Mkilanya alidia kuwa washtakiwa hao walikiuka maagizo yaliyotolewa na Kamati hiyo ya kutaka fedha hiyo iliyolipwa Simba kutoka  Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia, ifunguliwe akaunti maalum, lakini wao waliihamisha fedha hiyo kwenda katika akaunti ya mtu  binafsi.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 10, yakiwemo ya  kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uwongo na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila Kamati ya Utendaji ya Simba,kukaa kikao.

Katika mashitaka la kughushi linawakabili washitakiwa wote, anadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Pia katika mashitaka mengine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

Advertisement