Mavunde: Yanga bora inatengenezwa na Wanachama

Muktasari:

  • Mwenyekiti huyo alisema walikuwa na mipango maalum ya kuhakikisha kwamba zoezi hilo linaenda sawa kwa kusambaza kadi mikoa mbalimbali.

MWENYEKITI wa kamati ya kuchangisha pesa maalum  (hamasa) kwa klabu ya Yanga, Anthony Mavunde amewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo waendelee kuchangia kama kawaida.
Mavunde alisema tangu wameanza kuchangia imeonyesha kabisa kwamba klabu hiyo inaweza kujiendesha kupitia wanachama.
"Sisi tulikuwa na kazi ya kuchangisha pesa ili kumuwezesha kocha wetu asajili wachezaji anaowataka kwaajili ya msimu ujao, tulikuwa na mpango wa muda mfupi pamoja na muda mrefu ili Yanga iweze kujisimamia yenyewe," anasema.
Aliongeza "Wanachama na wapenzi wa Yanga ambao mlikuwa mnatoa mchango, kama mlikuwa mnatoa pesa mkawa mnajua ndogo basi nawaambieni mnatoa mchango mkubwa na leo mtasikia matunda yake".
MIPANGO YA MUDA MFUPI
Mwenyekiti huyo alisema walikuwa na mipango maalum ya kuhakikisha kwamba zoezi hilo linaenda sawa kwa kusambaza kadi mikoa mbalimbali.
"Tulikuwa tunasambaza kadi za milioni milioni na lengo lilikuwa watuchangie pesa hizo, pili ilikuwa lazima tufanye halfa fupi ya kuchangisha ili kupata pesa na malengo yote ni kutatua changamoto za wachezaji," anasema Mavunde.
Aliongeza asilimia kubwa watu wanaingiza pesa katika akaunti yao na mpaka sasa zoezi hilo linaendelea.