Mautundu ya Domayo kumbe sio uwanjani tu

Muktasari:

Kiungo Domayo amekuwa katika kiwango cha juu tangu alipoanza kucheza Ligi Kuu, amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya majeruhi ya mara kwa mara jambo, lakini haijakatisha uwezo wake wa kucheza soka la kiwango cha juu

Dar es Salaam. UFUNDI alionao na hasa uwezo wa kuchukua mipira na kuisambaza kwa ufasaha kwa wenzake kutokea eneo la kiungo kulimfanya Frank Domayo apachikwe jina la Chumvi na mashabiki wa soka waliovutiwa na soka lake.
Kama ilivyo kwa chumvi na umuhimu katika misosi, ndivyo Domayo alivyokuwa na alivyo muhimu uwanjani kwani yeye ni Chumvi kweli  anayelinogesha eneo la kati Kiungo huyo mwenye uwezo pia wa kucheza kama namba kumi, ameanza kurejea kwenye kile kiwango chake kilichopunguzwa awali na majeraha aliyokuwa nayo kwa muda mrefu.
Hans Pluijm anayeinoa Azam anatajwa kuwa nyuma ya kurejea kwa makali ya Domayo ambaye hivi karibuni aliitwa na kucheza timu ya taifa, Taifa Stars katika mechi za kuwania Afcon 2019 dhidi ya Uganda iliyoisha kwa suluhu mjini Kampala.
Mwanaspoti imeongea na Domayo aliyepo kwa sasa Afrika Kusini kwa matibabu ya majeraha aliyoyapata akiwa na Stars na kuweka bayana maisha yake ya soka ndani na nje ya uwanja na kuthibitisha kuwa utundu wake haupo uwanjani tu, hagta nje ya soka.

MJENGO WAKE
Asikuambie mtu, Domayo ni kati ya mastaa wasiri mno ambao hawapendi na hawataki kabisa kuweka mambo yao hadharani, licha ya kwamba wanafanya mambo makubwa nje ya uwanja.Hata hivyo Mwanaspoti lilivyo makini lilifika mpaka eneo la Kifuru, Mbezi pembezoni mwa jijini Dar es Salaam ambako ndiko mjengo wake upo na ndiko inakoishi familia yake.
Mjengo wake upo kilimani ni wa kifahari kweli kweli ni miongoni mwa nyumba ambazo zinasifiwa na mfano eneo hilo.
Katika mjengo huo Domayo anaishia na mkewe kipenzi sambamba na mwanae wa kiume Grayson pamoja na shemeji zake wa kike wawili.
Supastaa huyo hakutaka kutaja gharama ya mjengo huo, lakini ameweka wazi kwamba alitumia pesa za dau la usajili wake wa kutua Yanga na Azam FC kwa nyakati tofauti.
"Siwezi kusema dau,  ila nashukuru Mungu nina sehemu ya kuishi na familia yangu, nimefanya hayo yote kupitia soka sambamba na mengine ambayo yamenifanya niwe hivi nilivyo, kwa kweli namshukuru sana Mungu," anasema.

MWANAYE USIPIME
Domayo amejaliwa kupata mtoto wa kiume anayeitwa Grayson (3), anayetamani afuate nyayo zake za kupiga boli kwa madai hajawahi kujuta kuchagua soka maishani mwake.
"Soka limenipa heshima, limenipa hatua ya kimaisha kwa maana ya uchumi, hivyo sioni ubaya wa mwanangu Grayson kuwa mchezaji wa mafanikio zaidi yangu.
"Nikiwa nyumbani napata muda wa kumfundisha, naona anapenda kucheza, naomba Mungu afanikishe ndoto ninayotamani kwa mtoto wangu, natamani aje afike anga za kimataifa," anasema.

MAISHA AZAM
Maisha ya Azam kwa staa huyo yapo poa sana, kwani amekiri mambo yanaenda vizuri ambapo anaamini yanamfanya kiwango chake kuwa imara.
"Maisha ndani ya Azam FC, yapo vizuri naona hata kiwango changu kinakuwa siku hadi  siku, lakini pia baadhi ya vitu vyangu nafanikisha kwa wakati," anasema.
Domayo anafichua siri kubwa kwamba hata ndani ya Yanga alikuwa amejifunza mambo mengi ya kisoka na maisha ya kawaida.
"Yanga ina staili yake ya maisha kwa maana ina mashabiki wengi kupitia hao nilijifunza mengi yaliofanya niwe na mtazamo mpana kama mwanasoka," anasema.

KURUDI STARS
Domayo akiwa Yanga alikuwa habanduki katika kikosi cha Stars, tofauti na sasa ambapo anaitumikia Azam FC.
"Naamini nitakuwa na nafasi mbele ya Kocha Mnigeria Emmanuel Amunike, hivyo Watanzania wataendelea kuona mchango wangu kwa taifa letu wote," anasema anayekiri majeraha ya muda mrefu yalichangia kumuengua katika timu hiyo ambayo alirejeshwa tena na Amunike baada ya baadhi ya mastaa wa Simba kutimuliwa kwa kuchelewa kambini kabla ya kusamehewa.

ANAYEMKUBALI
Nyota huyo wa zamani wa Yanga, anasema amekuwa akivutiwa na kiwango cha Kiungo wa kimataifa wa Croatia na Real  Madrid, Luka Modric ambaye hivi karibuni alitwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa FIFA.
Domayo anasema Modric ni kiungo pekee ambaye amekuwa akijifunza mengi kutoka kwake toka alipokuwa akiichezea Tottenham Hotspur ya England.
"Nampenda Modrick kwa aina ya uchezaji wake, jamaa ana uwezo wa kupiga pasi karibu, lakini ni mzuri kwenye pasi za mbali kama timu inashambulia kwa kustukiza."

MALENGO YAKE
Kama unadhani Domayo kafika mazima Azam FC utakuwa umekosea njia, mawazo yake ni kukipiga nje ikiwa ni moja ya ndoto zake za muda mrefu.
"Sitaki kustaafia soka kwenye Ligi Kuu Bara, kwani  nawaza kucheza nje ya nchi, siwezi kuitaja ni wapi ila popote nitakapopata nafasi naamini nina uwezo wa kucheza nje ya nchi tena kwa mafanikio kwa kipaji nilichojaliwa na Mungu."

WASIFU WAKE:
Jina:Frank Domayo
Kuzaliwa: Feb 16, 1993
Mahali: Dar es Salaam
Uraia: Tanzania
Nafasi: Kiungo
Timu: Azam FC
Jezi: Namba 18
Alikopita: JKT Ruvu, Yanga