Maugo ajitosa BMT kupinga uamuzi wa Kamisheni ya ngumi

Friday July 12 2019

 

By Imani Makongoro

BONDIA Mada Maugo yuko mbioni kutinga Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupinga uamuzi wa Kamisheni ya ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kumpa ubingwa wa Tanzania, Twaha Kiduku.
Pambano la mabondia hao lililofanyika mkoani Morogoro lilivunjika baada ya Maugo kudaiwa na refarii, Pembe Ndava kwamba alicheza faulo.
Hata hivyo, hakuna bondia aliyetangazwa bingwa katika pambano hilo hadi hivi karibuni baada ya kikao cha TPBRC ambacho kilimpa ubingwa huo  Kiduku.
"Sijaridhika na uamuzi wa Kamisheni, binafsi naona kama sijatendewa haki na sikuitwa wakati wakichukua hatua hizo," alisema Maugo.
Alisema atapeleka malalamiko ya BMT kwani ni kama mpinzani wake amepewa ushindi wa mezani wakati hakustahili.
"Niliambiwa na viongozi wawili wa TPBRC kuwa huo ndiyo uamuzi wa kamisheni, madai yaliyokuwepo ni kwamba mimi nilimpiga ngumi mpinzani wangu chini ya mkanda, lakini kabla ya pambano hatukusomewa sheria za ubingwa huo.
"Isitoshe katika ngumi bondia anapopigwa chini ya mkanda akilalamika anapewa dakika tano za uangalizi, lakini kwa Twaha, refarii kwa utashi wake tu ndiyo aliamua kumaliza pambano," alisema.
Alidai kingine ambacho kinamfanya aende BMT ni majibu aliyopewa na Kamisheni kwamba Kiduku hawezi kutetea ubingwa huo na bondia mwingine hadi warudiane na Maugo.
"Binafsi sijaridhika na uamuzi huo wa Kamisheni, kabla ya hukumu ilipaswa marefa waitwe waangalie video ya pambano kabla ya kutoa uamuzi ambao naona kama hayo hayakufanyika na sikutendewa haki ndiyo sababu nahitaji nakala ya hukumu ili nipeleke malalamiko yangu BMT," alisema.
Makamu wa Rais wa TPBRC, Aga Peter alisema, uamuzi wa Kamisheni haukuwa wa kubahatisha kumpa ubingwa Kiduku.
"Maugo alicheza faulo nyingi katika pambano lile, hata refarii tulimlaumu kwa kuchelewa kulimaliza, halafu si kweli kwamba ameambiwa hakuna bondia ambaye atacheza na Kiduku hadi watakaporudiana," alisema.


Advertisement