Matumla ampa mbinu bondia Mtango

Muktasari:

Mtango ambaye ameweka kambi Dar es Salaam chini ya bingwa huyo wa zamani wa dunia wa WBU amekuwa na programu maalumu ya kujifua kwa saa sita kila siku.

Dar es Salaam. Baada ya kumsimamia mazoezi kwa wiki mbili, Rashid Matumla ambaye ni kocha wa Salum Mtango amesema ubingwa wa bondia huyo utaamuliwa na utulivu wake ulingoni.

Mtango atapanda ulingoni Januari 31 kumkabili Suriya Tatakhun wa Thailand katika pambano la raundi 12 la ubingwa wa dunia wa Universe Boxing Organisation (UBO). Pambano hilo la uzani wa super feather litapigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga likitanguliwa na mengine sita.

Mtango ambaye ameweka kambi Dar es Salaam chini ya bingwa huyo wa zamani wa dunia wa WBU amekuwa na programu maalumu ya kujifua kwa saa sita kila siku.

Akizungumza jana, Matumla alisema Mtango anafanya mazoezi mara tatu kwa siku. “Amefanya mazoezi ya mbinu, ufundi, pumzi na kupigana ana kwa ana (sparing), kilichobaki ni Mtango kufanya kile alichoelekezwa na kucheza kwa utulivu,” alisema nguli huyo.

Alisema utulivu ndio utambeba bondia huyo ambaye kama atashinda atapanda viwango vya ngumi duniani kutokana na rekodi ya mpinzani wake ambaye ana nyota mbili. Mthailand huyo ana historia ya kuwachapa Amos Mwamakula, Fred Sayuni na Sadiki Momba kwa TKO na KO.