Matumla, kocha wa Mwakinyo kibaruani kuleta ubingwa wa dunia

Muktasari:

Mtango  ametamba kuwa Mthailand ajipange kwani anaamini mazoezi atakayopata katika jopo la makocha wake waiongozwa na Rashid Matumla yatamkalisha mpinzani wake raundi za awali.

Dar es Salaam.Bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla na Hamis Mwakinyo ni makocha watakaomnoa Salum Mtango anayejiandaa kuwania ubingwa wa dunia wa Universe Boxing Organisation (UBO).
Mtango atazichapa na Amnat Ruenroeng wa Thailand,pambano la uzani wa super feather la raundi 12 litakalopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga Januari 31 mwakani.
Promota wa pambano hilo, Ally Mwanzoa amesema maandalizi  yanakwenda  vizuri ambapo litatanguliwa na mapambano mengine sita.
"Tunaamini Mtango atafuata nyayo za  kaka zake wenye rekodi ya kuwapiga Knock Out (KO) mbaya mabondia wa Thailand akiwamo Magoma Shabani.
"Itakuwa fedhea kama Mtango atapoteza ubingwa huu, lakini kwa maandalizi ambayo anaendelea kufanya chini ya jopo la makocha atafanya vizuri na kubakisha ubingwa nyumbani, " amsema
 Mwanzoa ambaye amewahi kuwa promota wa Hassani Mwakinyo.
Akizungumzia maandalizi yake, Mtango amesema yuko chini ya jopo la makocha wanne wakiongozwa na Matumla (Snake man) na Hamis Mwakinyo.
"Hakuna shaka , uwezo wa makocha hao kwenye ngumi kila mmoja anaufahamu, hivyo Mthailand ajipange," alijinasibu Mtango aliyepiga kambi mkoani Tanga.
Aliwaomba Watanzania, Serikali kupitia wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo chini ya Waziri, Dk Harrison Mwakyembe, Taasisi na wadau wa kampuni kulisapoti pambano hilo.
Kocha Matumla alisema anamuandaa Mtango kufuata nyayo zake katika ngumi na Watanzania wasiwe na hofu ya ubingwa huo kubaki nyumbani.
"Sikuwa na kazi mbovu enzi zangu, hivyo Mtango pia nahitaji afuate nyayo zangu, najua namna ya kuwatengeneza vijana, hivyo Watanzania wajiandae kupokea ubingwa" alisema Matumla aliyeng'ara enzi zake kimataifa kwenye uzani wa super welter.