Matola alia ratiba kumnyima pointi tatu kwa Mbao

Muktasari:

Mbao wamecheza mechi 10 na kuvuna pointi 17 na kukaa nafasi ya sita, huku Lipuli wakiwa wameshuka dimbani mara tisa na kukusanya alama tisa na kukaa nafasi ya 14.

Mwanza. Kocha wa Lipuli FC, Seleman Matola amesema kutokana na mabadiliko ya ratiba ya mchezo wao dhidi ya Mbao uliopangwa awali kupigwa Alhamisi na baadaye kusogezwa nyuma kuchezwa kesho Jumatano huenda ikawapa wakati mgumu kupata pointi tatu.
Mbao inatarajia kuwakaribisha 'Wanapaluhengo' hao katika mchezo wa raundi ya 11 wa Ligi Kuu, utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Akizungumza baada ya mazoezi yao leo jioni Kocha Matola amesema ratiba haipo rafiki kwao kutokana na kuchoka kwa vijana wake kwani walijua mechi yao itapigwa Alhamisi na kubadilishwa kuchezwa kesho Jumatano.
Ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko hayo hawana jinsi badala yake ni kupambana kusaka pointi tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri.
"Ni kweli ratiba si rafiki na inaweza kutusababishia kutopata matokeo mazuri kutokana na uchovu kwa vijana wangu, lakini tutapambana kuwakabili wapinzani kuhakikisha tunashinda" amesema Matola.
Kocha huyo amesema atawakosa wachezaji wanne ambao wana matatizo tofauti, ikiwa ni Malimi Busungu ambaye ametoweka kinyemela na hajulikani halipo, Joseph Owino mwenye matatizo ya kifamilia, Jamali Mnyate na Freddy Tangalu aliyeumia mechi iliyopita.
"Niwaombe wadau na mashabiki kutuombea na tumejipanga kutowaangusha,nimewaandaa vijana wangu kiushindani kwa sababu nawajua Mbao wamekuwa na mwanzo mzuri kwenye Ligi," amesema Kocha Matola.