Matola, Zahera kuvaa buti la Djuma Simba

Muktasari:

Yanga ya Kocha Mwinyi Zahera imekaa kileleni kibabe ikikusanya alama 50 katika mechi 18. Zahera aliyenyakua tuzo tatu za Kocha Bora wa Ligi Kuu kwa miezi ya Septemba, Novemba na Desemba.

HUENDA taarifa hii isiwavutie sana mashabiki wa Yanga, lakini ndivyo ukweli ulivyokuwa, Kocha Mwinyi Zahera na Seleman Matola mmoja ndiye atakayemrithi Djuma Masoud ndani ya Simba baada ya majina yao kuwa mezani mwa mabosi wa Msimbazi.

Zahera huyu huyu mnayemjua aliyeiwezesha Yanga kukaa kileleni kibabe ikikusanya alama 50 katika mechi 18. Zahera aliyenyakua tuzo tatu za Kocha Bora wa Ligi Kuu kwa miezi ya Septemba, Novemba na Desemba.

Ipo hivi. Habari kutokana ndani ya Simba zikimkunukuu mmoja wa vigogo zinasema kuwa, Matola na Zahera ndio wanaochuana ili kuchukua nafasi ya ukocha msaidizi iliyoachwa na Masoud aliyetimkia AS Kigali ya Rwanda.

“Kuhusu kocha msaidizi, tunatarajia kukutana na Kocha Mkuu, Patrick Aussems, lakini ukweli mezani kwetu kuna majina mawili tu kwa sasa, Matola na Zahera. Unajua fedha ina uwezo wa kufanya lolote, hivyo subirini maamuzi ya mwisho,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya Simba.