Matokeo ya Uchaguzi Mkuu Simba yatangazwa

Muktasari:

  • Uchaguzi huo wa jana yalikuwa ni zoezi hilo kufanywa na idadi ya wanachama takribani 1500 lakini jana jumla ya wanachama 1728 walijitokeza kwa ajili ya kutimiza haki yao ya kikatiba ya kushiriki Mkutano Mkuu na kuchagua viongozi wao.

Dar es Salaam.Wakati wanachama wa Simba wakiandika historia kwa kufanya uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa kampuni ambao utaendesha klabu yao huku Swedi Nkwabi akichaguliwa kwa kishindo kuwa mwenyekiti sambamba na wajumbe watano, klabu hiyo imetangaza bajeti ya zaidi ya Shilingi 6 bilioni kwa ajili ya msimu wa 2018/2019.
Nkwabi alishinda nafasi hiyo ya uenyekiti baada ya kupata zaidi ya 51% ya kura zote zilizopigwa na wanachama wa klabu hiyo wapatao 1728 waliohudhuria mkutano huo uliofanyika kwenye kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere kilichopo Posta Mpya jijini Dar es Salaam jana.
Idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Simba ambao ulikuwa sehemu ya ajenda za Mkutano Mkuu wa klabu hiyo jana tofauti na akidi iliyotegemewa kuhudhuria siku chache kabla ya mkutano huo, ilionyesha wazi kiu na hamu ya kila mwanachama kuwa sehemu ya historia ya klabu hiyo kupitia mchakato huo wa jana.
Awali matarajio ya kamati ya Uchaguzi ya Simba siku chache kabla ya Uchaguzi huo wa jana yalikuwa ni zoezi hilo kufanywa na idadi ya wanachama takribani 1500 lakini jana jumla ya wanachama 1728 walijitokeza kwa ajili ya kutimiza haki yao ya kikatiba ya kushiriki Mkutano Mkuu na kuchagua viongozi wao.
Uchaguzi ulivyoendeshwa
Baada ya mkutano mkuu wa Simba kumalizika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere Kamati ya Uchaguzi aliyekuwa Kaimu Rais Salim Abdallah 'Try Again' alipofunga mkutano mkuu wa mwaka alimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Boniface Lyamwike.
Kamati ya Uchaguzi ilikabidhiwa kijiti saa 06:40 mchana huku wanachama wakitakiwa kuchagua viongozi watakaoifanya Simba Sports Club Limited kufika wanakohitaji.
Kaimu rais wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' ndiye aliikaribisha kamati ya Uchaguzi iliyoongozwa na huku akisisitiza wakati huo ndiyo mahali pekee palipokuwa panasubiriwa na Wanasimba ili kutengeneza mustakabali wa klabu yao.
Huku akishangiliwa, Try Again alisema Simba inahitaji kiongozi ambaye ataisaidia klabu siyo yeye asaidiwe na klabu, haitaki kiongozi wa historia kuwa alifanya hiki au kile bali Simba inahitaji kiongozi msafi kiutendaji.
Try Again aliwambia wanachama wawe makini katika zoezi hilo kwani jukumu ni lao, wasifuate upepo katika kuchagua viongozi.
Baada ya kukabidhiwa kijiti, Lyamwike alianza kutambua uwepo wa viongozi mbalimbali wa klabu hiyo huku akisisitiza zoezi analokwenda kulisimamia litakuwa la kuitoa Simba kutoka ile ya asili hadi ya hisa.
Alisema mwanzoni Simba ilikuwa ni mpira lakini sasa inakwenda kufanya mpira na biashara hivyo watakaochaguliwa wajue namna ya kutengeneza mipango ya kuiletea Simba faida
Lyamwike aliharibu hali ya hewa ukumbini hapo baada ya kuwatangazia wanachama kwamba akida ya wapiga kura imeongezea tofauti na ile aliyoitangaza awali.
Awali akidi iliyotangazwa ilikuwa ni wanachama 1720 lakini wajumbe nane wa mkutano huo waliongezeka jambo lililozua taharuki kwa wagombea na wanachama wakionyesha kutoridhiswa na ongezeko hilo la ghafla la wapiga kura.
Kaduguda awasha moto, wanachama wamtuliza
Mgombea ujumbe Mwina Kaduguda hakufurahishwa na ongezeko hilo na kuanza kuhoji ni kwa vipi wanachama hao nane walioongezeka waruhusiwe kuingia na kufanya idadi ya wanachama iwe 1728 badala ya ile 1720 wakati mlango umefungwa hapo ndipo majibizano yalipoanza.
Baada ya kutolewa nje kulizuka sekeseke ambapo mgombea huyo alijibu kwa kujiamini kwamba ni haki yake kuhoji idadi ya wagombea kutoka 1720 hadi 1728.
Lyamwike aliamua kuomba msaada kwa askari polisi waliokuwepo ukumbi hapo ili kumtoa nje Kaduguda ambaye alikuwa ametoka kwenye kiti alichokaa na kwenda kulalamika kwenye meza kuu.
Nje ya ukumbi, Kaduguda alionekana kutaka kususia uchaguzi huo na kurejea nyumbani lakini baadhi ya wanachama walimuwahi na kumsihi abadili maamuzi yake na kurejea ukumbini kushiriki zoezi hilo.
Baada ya tukio hilo, watu wa usalama askari polisi walikwenda kumtoa na kumpeleka nje akiwa analalamika na kuhoji alitolewa kwa sababu gani wakati alitimiza haki yake ya kuhoji baada ya kutilia shaka uamuzi huo, jambo ambalo lilipelekea pia wagombea wote waliobaki kutolewa nje kwa ajili ya kufanya mazungumzoa kabla ya kurejea ukumbini wakiwa wameambatana na Kaduguda.
Kaduguda alirejea ukumbini akisindikizwa na baadhi ya wanachama na Polisi mmoja na moja kwa moja alienda meza kuu na kukumbatiana na Kaimu Rais wa Try Again na kuamsha shangwe kutoka kwa wanachama.
Alipohojiwa na gazeti hili kwa uamuzi wake wa kutotaka kususia, Kaduguda alisema "Kuna makubaliano tulikubaliana na Mwenyekiti wa kamati, lakini niliona yale makubaliano ya wote Mwenyekiti alionekana anayapindisha ndio maana nilienda kuhoji.
"Sikuona sababu ya kuendelea kuwepo kwenye uchaguzi kwani nina misimamo yangu ambayo naisimamia," alisema Kaduguda
Abadili upepo akiomba kura
Tofauti na ilivyotarajiwa, Kaduguda alibadili upepo kwa wagombea baada ya kujieleza kwa mikwara huku wajumbe wakifurahia hotuba yake.
Kaduguda ambaye pia aliwahi kuwa katibu mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), alianza kujinadi kwa kuelezea wasifu wake na kugomea kujiita msomi huku akitaka aitwe mwanazuoni.
Huku wagombea wakionekana kufurahia kujinadi kwake tofauti na awali ambapo baadhi yao walimzomea alipogomea akidi, Kaduguda alidai ana shahada ya mpira wa miguu aliyoipata bara la Ulaya.
"Nimejifunza mpira kule Budapest Hungary. Najua mpira, nI mweledi,muadilifu na mwenye msimamo, ninayestahili kuwa kwenye bodi ya Wakurugenzi ya Simba," alijinasibu Kaduguda.
Jasmine, Tully wapata changamoto
Wagombea Jasmine Badour na Said Tully walikumbana na changamoto ya maswali kutoka kwa wanachama ambao walitaka kujua mambo waliyoyafanya wakiwa kwenye uongozi uliomaliza muda wake na kinachowapeleka kugombea tena.
Jasmine ambaye ni mke wa nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Victor Costa na Tully walijikuta wakipigwa maswali matano kila mmoja ingawa utaratibu ulikuwa ni kila mgombea kuulizwa maswali matatu.
Mgombea huyo wa nafasi ya ujumbe kwa wanawake ndiye alipata wakati mgumu zaidi kuliko Tully kwani kadri alivyokuwa anajibu ndivyo wanachama walivyozidi kunyoosha mikono kuomba ridhaa ya kumuuliza maswali.
Hata hivyo yeye na Tully walipangua baadhi ya maswali huku mengine yakitupiliwa mbali kutokana na kukosa mashiko, ingawa pamoja na hilo, baadhi ya wanachama walionyesha kutoridhishwa na majibu yake.
Wakati Jasmine akihangaika kujibu maswali, mgombea mwenzake, Asha Baraka alipata mchekea kwa kutoulizwa swali hata moja.
Mbali na hao, wagombea wengine walipata fursa ya kujinadi na kuomba kura kwa umati wa wanachama waliohudhuria.
Kamati kukabidhiwa kijiti
Mwongozo kupiga kura
Kamati ya Uchaguzi chini ya Lyamwike Ilitoa muongozo kwa wapiga kura muda mfupi kabla ya zoezi la kupiga kura kwenye Uchaguzi mkuu kwa kuwaelekeza wapiga kura jambo la kufanya.
Alisema wapigakura wataraliwa kuchagua wajumbe watano pekee kati ya wagombea 17 na sheria inasema mmoja kati yao lazima awe mwanamke
"Mtapewa Fomu mbili mkononi, moja ya Mwenyekiti (mgombea mmoja)  na nyingine ya wajumbe,"
Alisema zoezi la kuhesabu kura ni la kamati na hawatoruhusu mtu yoyote kuwasaidia.
Alisema mgombea ndiye anayeujua uchungu wa nafasi anayoigombea, hivyo yeye ndiye atasimamia kura zake au mtu anayemuamini {wakala)
Mkutano wapitisha bajeti tishio
Awali kabla ya zoezi la Uchaguzi kufanyika, wanachama wa klabu hiyo waliosomewa bajeti ya Sh 6 bilioni ambayo itatumika kwa msimu wa 2018/2019 huku pia wakisomewa taarifa ya mapato na matumizi na mhasibu wa klabu hiyo, Amos Gahumeni.
Gahumeni aliibua nderemo na vifijo baada ya kutangaza kuwa katika bajeti hiyo ya Sh 6 bilioni, nyota wa kikosi cha Simba watapatiwa kiasi cha Sh 400 milioni kama bonasi iwapo watafanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Kwa mujibu wa Gahumeni, msimu uliopita klabu ya Simba ilipata kiasi cha Sh 4,98 bilioni kutoka kwenye vyanzo vyake mbalimbali vya mapato na matumizi yake yalikuwa ni kiasi cha zaidi ya Sh 5.31 bilioni ikimaanisha walipata hasara ya zaidi ya Sh 800 milioni.
Magori aula
Mkutano huo Mkuu wa klabu ya Simba mbali ya kutangaza bajeti hiyo ya kibabe, jana ulimtaja aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Clescentius Magori kuwa Mtendaji Mkuu (CEO)  wa klabu hiyo chini ya mfumo wa uwekezaji wa kampuni ambao ndio unaiendesha klabu hiyo kwa sasa baada ya kufanya mabadiliko ya katiba yake.
Kaimu Rais wa Simba 'Try Again alimtangaza Magori na kusema ataongoza bodi ya klabu hiyo itakayokuwa na muunganiko wa wajumbe kutoka upande wa klabu ambao ni wawakilishi wa wanachama pamoja na upande wa mwekezaji.
Try Again alimtaka Magori  kuhakikisha Simba inatawala kisoka  Afrika kama moja ya majukumu yake kwani hivi Sasa klabu hiyo haina tatizo la fedha na kilichobaki mpira uchezwe .
"Hivi Sasa tunakoelekea pesa ipo hivyo uhakikishe Simba inatawala si Tanzania Bali Afrika"alisema Abdallah na wanachama kupiga makofi.
Magori amewahi kuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii(NSSF).
Kilomoni awasapraizi wanachama
Katika hali ya kushangaza, mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Simba, Mzee Hamis Kilomoni jana alitinga kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere ambako kulifanyika Mkutano huo Mkuu wa Simba, na kushangiliwa na umati wa wanachama.
Mzee Kilomoni alikuwa ni miongoni mwa wanachama wa klabu hiyo ambao walikuwa wakipinga mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wake na ilifikia hatua hadi ya kufungua kesi mahakamani.
Umati wafurika mkutanoni
Tofauti na akidi iliyotangazwa awali kuwa mkutano huo utahudhuriwa na wanachama takribani 1,500, jumla ya wanachama 1728 walijitokeza kushiriki mkutano huo hali iliyopelekea kukosekana kwa viti vya kukalia na kusababisha wakae chini kufuatilia mkutano huo.
Pamoja na mshehereshaji (MC) kuwataka wanachama hao kutoziba njia zab ukumbi kwa kukaa chini, wanachama walipaza sauti wakimlalamikia MC kuwa hawana mahali pa kukaa hivyo waachwe wasibughudhiwe.
Ratiba yawachefua wanachama
Kuchelewa kuanza kwa mkutano mkuu wa Simba kuliwakera wanachama wa klabu hiyo ambao walidai ingewabana.
Ratiba ya kufungua mkutano mkuu ilionyesha kuanza saa 3:25 kwa Mwenyekiti kufungua mkutano mkuu ambayo ingefanyika hadi saa 6:30 mchana.
Hadi saa 4:15 asubuhi, mkutano haukuwa umeanza huku baadhi ya wanachama ambao waliomba hifadhi ya majina yao wakilalamika kuwa kuchelewa kuanza kwa mkutano huo kama ratiba ilivyopangwa kutasababisha waburuzwe Katiba baadhi ya ajenda hususani ya mapato na matumizi.
"Tuna mkutano miwili, hadi sasa hakuna kinachofanyika, hii si dalili nzuri katika ajenda za mkutano mkuu kwani tuko nyuma ya muda na inaonyesha kuna baadhi ya ajenda hususani ya mapato na matumizi tutaburuzwa," alisema mmoja wa wajumbe ambaye aliungwa mkono na wenzake ndani ya ukumbini wa JNICC.
Vigogo kibao wahudhuria
Mbali na umati mkubwa ya wanachama waliohudhuria, viongozi na wadau wengi maarufu wa klabu hiyo walijitokeza kushiriki kwenye mkutano huo wakiongozwa na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah 'tRY Again', Zacharia Hanspoppe, Juma Kapuya, Hassan Dalali, Mulamu Nghambi, Hassan Hassanoo na wengineo.
Hassanoo asisimua wanachama
Hassan Hassano aliamsha shangwe katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere baada ya kutambulishwa.
Hassano ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba  alihudhuria mkutano huo.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alikuwa akitambulisha watu mbalimbali maarufu na wanachama kupiga makofi lakini alipofika kwa  Hassanoo alimtambulisha na kuchombeza kuwa mpiganaji na  wanachama walilipuka kwa makofi mengi zaidi.
Kagere atajwa mkutanoni
Mshambuliaji Meddie Kagere ni mchezaji pekee aliyetajwa kwenye mkutano mkuu wa wanachama baada ya Manara kuwaambia wanachama kuwa wachangamke kwani Simba siyo timu ya mchezo mchezo.
"Kagere anawakimbiza tu huko uwanjani, halafu mnakuwaje wanyonge embu changamkeni buana," alisema Manara huku akikoleza kauli yake kwa kutamka kauli mbiu ya Simbaaa, na wanachama kuitikia kwa nguvu wakishangilia, Nguvu moja.
Ulinzi watawala
Askari Polisi wengi walimwagwa ndani na nje ya Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Posta unakofanyika mkutano mkuu wa Uchaguzi wa Klabu ya Simba.
Mitandao na magazeti yetu ilishuhudia Askari mbalimbali wakiranda nje ya Ukumbi huo na wengine ndani wakihakikisha usalama unakuwepo ambapo kuna waliovaa sare na wale waliovaa kiraia.
Askari wengine walionekana wakiwa kwenye magari yao ya wazi wakiwa na silaha na kuimarisha ulinzi kwa kila anayeingia na kutoka katika Ukumbi.
Kauli ya JPM ndani ya mkutano Simba
Kauli ya Rais John Pombe Magufuli imekolezwa kwenye mkutano mkuu na Uchaguzi mkuu huo wa Simba uliofanyika jana.
Katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa klabu hiyo, Manara alisema klabu imeagizwa na rais kutwaa ubingwa wa Afrika hivyo kazi ndiyo inaanza.
"Ni klabu moja tu pekee ambayo imeagizwa na rais kuleta ubingwa nayo ni Simba, hivyo kazi ndiyo inaanzia hapa," alisema Manara huku akishangiliwa kwa nguvu na wanachama.
"Rais Magufuli alitoa tamko la kuitaka Simba itwae ubingwa alipokwenda kwenye mechi ya mwisho ya Ligi kati ya Simba na Kagera Sugar ikiwa ni mara yake ya kwanza kwenda kwenye mechi za Ligi Kuu tangu alipochaguliwa kuwa rais Oktoba 2015," alisema Manara
Imeandikwa na Mwanahiba Richard, Imani Makongoro, Thobias Sebastian, Oliver Albert na Doris Maliyaga.