Matibabu ya haraka kwa jeraha la MO Salah haya!

MSHAMBULIAJI hatari wa Liverpool, Mohamed Salah hakupangwa katika mchezo wa Jumanne wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Barcelona. Hii ni kutokana na majeraha ya kichwa aliyoyapata.

Salah alipata majeraha hayo katika mchezo mkali wa Ligi Kuu England walioshinda mabao 3-2 dhidi ya Newcastle United uliopigwa Ijumaa ya wiki iliyopita.

Ilikuwa ni dakika ya 73 kipindi cha pili alipogongana na mlinda mlango wa Newcastle, Martin Dubravka aliyekuwa katika harakati za kudaka mpira wa juu huku Salah naye akikwea hewani ili kuwania mpira huo.

Mgongano huo ndio uliosababisha Salah kugongwa eneo la kichwani na kupata tatizo lijulikano kitabibu kama Brain Concussion, yaani jeraha la mtikisiko wa ubongo hivyo kumlazimu kutolewa nje kwa machela.

Aina hii ya jeraha la ubongo huweza kumsababishia mchezaji kupoteza fahamu, kichwa kuuma, kuweweseka, kupata kizunguzungu na kuchanganyikiwa.

Bahati nzuri Mo Salah alipata ajali hiyo bila ya kupoteza fahamu zaidi tu alionekana kuwa na maumivu makali ya kichwa na kuweweseka kidogo.

Aina hii ya majeraha yanapotokea mchezaji huhitajika kuwa katika uangalizi maalumu wa wataalamu wa afya kwa saa 24-48 na mapumziko ya muda marefu.

Hutakiwa kuepukana na aina yoyote ya mambo yanayoweza kumtikisa au kumsababishia kuwa katika hatari ya kujijeruhi tena ikiwamo michezo inayohusisha mwili ikiwamo mpira wa miguu.

Hivyo, kwa hali ya Salah aliyokuwa nayo pamoja na kuonekana uwanjani akiwa mzima wa afya kama mtazamaji Jumanne, lakini asingelikuwa rahisi kuchezeshwa mechi ile iliyokuwa na ushindani.

Ndani ya saa moja tangu kutolewa uwanjani alifanyiwa uchunguzi wa kina ikiwamo picha za X-ray na CT Scankuona kama kuna damu yoyote ambayo imevilia katika ubongo au kuvunjika kwa fuvu.

Habari njema hapakuwa na matatiazo kama hayo. Baada ya matokeo haya hapakuwa na matibabu makubwa zaidi ya kutakiwa kupata mapumziko ya muda mrefu ili kutoa nafasi ya ubongo kupata utulivu.

Alikuwa chini ya uangalizi wa karibu wa saa 48 ambazo zilipita bila kuonyesha mabadiliko yoyote ya kiafya jambo ambalo kitabibu lilikuwa ni ishara ya kuwa na maendeleo mazuri kiafya.

Maendeleo haya ndiyo yaliyochangia kupewa ruhusa na jopo la madaktari kwenda kama mtazamaji katika mchezo huo wa nusu fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya UEFA, dhidi ya Barcelona.

mtikisiko wa ubongo

Kwa kawaida kuna aina tatu ya majeraha ya ubongo ambayo huwapata wanadamu kutokana na ajali mbalimbali ikiwamo ajali za michezoni kama aliyopata Salah.

Aina ya kwanza ndiyo aliyopata Salah inayojulikana kitabibu kama Concussion yaani mtikisiko, aina ya pili ni kuvimba kwa ubongo kitabibu hujulikana kama Brain Concussion na aina ya tatu ni mchaniko wa ubongo kitabibu hujulikana kama Brain Laceration.

Aina ya kwanza, concussion, ndiyo ambayo mara kwa mara inawapata wanasoka baada ya kugongana au kugongwa au kuanguka vibaya na kutua na kichwa.

Aina hii imeainishwa katika makundi matatu yaani kupata mtikisiko wa ubongo kwa kugongwa moja kwa moja na kitu kichwani, aina ya pili ni ubongo kusereka mbele au nyuma kutokana na shinikizo na aina ya tatu ni kutokana na mpasuko wa kitu uliotoa shinikizo kubwa.

Hivyo, kutokana na uanishaji wa majeraha haya jeraha la Salah ni aina ya kwanza ya jeraha la ubongo lililoainishwa kama mtikisiko wa ubongo kundi la kwanza.

Kwa kawaida aina ya pili na ya tatu ya majeraha ya ubongo ndiyo huwa na madhara makubwa na hata kifo kinaweza kutokea.

Ingawa hata aina ya kwanza ni kawaida kuwa na madhara yanayoweza kujitokeza ndani ya saa 24 au hata baadaye baada ya kupita siku kadhaa.

Madhara hayo ni pamoja na maumivu ya kichwa, kupoteza fahamu, degedege, kizunguzungu, kushindwa kutulia au kukosa umakini, kutoona vizuri, kuchanganyikiwa na kusikia milio ya kengele masikioni.

Kwa Salah mpaka sasa hakuna madhara haya yaliyojitokeza hivyo kuzidi kutoa ishara kuwa maendeleo yake ni mazuri.

Huduma ya kwanza

Majeraha ya ubongo aina ya concussion huweza kupona yenyewe bila matibabu ya juu. Mgonjwa hutakiwa kupata mapumziko yakutosha ili kupumzisha mwili na akili. Huzuiwa kucheza, kusoma, kuangalia TV, kutumia simu, computer, kuwasiliana na watu wengine kwa namna yoyote ile.

Huwa ni kawaida katika eneo la tukio kupata huduma za kwanza za dharula. Salah alipewa huduma ya kwanza kwa kiwango cha juu pale pale uwanjani na kubebwa kwa umakini wa hali ya juu lengo ni kujihami endapo jeraha ni kubwa katika ubongo au uti wa mgongo.

Jeraha la kichwani hasa michezoni yanaweza kuhusisha pia majeraha ya uti wa mgongo katika eneo la shingoni ndiyo maana Salah aliwekewa kifaa cha kutuliza eneo la shingo na kichwa. Ubebaji mbaya wa majeruhi wa ajali za michezo zilizohusisha majeraha ya uti wa mgongo huweza kusababisha majeraha zaidi na mjeruhiwa huweza kupooza. Katika kongamano la kimataifa lililofanyika nchini Zurich mwaka 2012 la umoja wa madaktari wa majeraha ya kichwani duniani kwa wanasoka walikuja na mapendekezo mbalimbali ili kukabiliana na tatizo la majeraha haya na Fifa waliyafanyia kazi.

Mapendekezo hayo ni pamoja na uboreshaji wa huduma ya kwanza viwanjani. Marefa walitakiwa kuwalinda wachezaji mara wanapoona amejeruhiwa vichwani ndiyo maana husimamisha mpira na kuita watoa huduma ya kwanza haraka.

Matibabu ya majeraha ya kichwa ni hatari hivyo mara nyingi matibabu ya msingi huanzia palepale uwanjani.

Madaktari wa majeraha ya michezo aliyekuwapo uwanjani huchukua hatua za haraka na kuuchunguza kwa namna alivyoliona tukio zima. Mara nyingine hata X-Ray huweza kutumika kubaini kama mfupa wa fuvu la kichwa umepasuka. Kama kuna damu imevuja huweza kuonekana kirahisi na hatua za kuiondoa damu hiyo kwa njia za upasuaji hufanyika haraka.

Hatma ya Salah

Mpaka kufikia leo taarifa za madaktari wa Liverpool zinaonyesha mchezaji huyo yuko fiti kucheza mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu dhidi ya Wolves hapo keshokutwa.

Hata kama hatapangwa keshokutwa lakini ana uhakika wa kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Totenham itakayopigwa jijini Madrid Hispania Juni Mosi 2019.

Kadiri anavyopumzika ndivyo afya yake inavyoboreka, hivyo ni vizuri kujifunza kuwa mwenye majeraha kama ya Salah hupumzishwa baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina.