Matatizo ya kifamilia yamuondoa Ninje, TFF

Muktasari:

  • Kwa muda nilikuwa pale TFF, nimefanya kazi nyingi na nimeacha alama kama Taifa Stars haijafuzu Afcon kwa muda mrefu, lakini chini yangu imewezekana

Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Wallace Karia ametangaza kuachana na Mkurugenzi wa ufundi shirikisho hilo Ammy Ninje.

Karia aliyasema hayo katika tukio la kutambulisha jezi mpya za timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kuwa Ninje hatakuwa tena Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho hilo.

Karia alisema wameamua kuachana na Ninje kutokana amekuwa na matatizo ya kifamilia yake inayoishi England.

"Atakwenda kusoma na kuangalia familia yake kwa ukaribu England kwa sababu hizo tumekubaliana kuachana naye katika nafasi hiyo," alisema Karia.

"Hatuna shida yoyote kati yetu na tumeachana kwa amani kutokana na kazi kubwa ambayo ameifanyia shirikisho," alisema Karia.

Akizungumza hali hiyo, Ninje alisema ameamua kutoka katika nafasi hiyo kutokana na matatizo ya familia yake.

Ninje aliyewahi kuwa kocha wa Ngorongoro Heroes, alisema nimeomba kurudi Uingereza kwenda kukaa karibu na familia yangu ili kumaliza hayo matatizo.

"Nimeondoka katika nafasi hii bila ya kuwa na tatizo na mtu yeyote hata maneno ambayo yanaongolewa si ya kweli," alisema Ninje.

"Kwa muda nilikuwa pale TFF, nimefanya kazi nyingi na nimeacha alama kama Taifa Stars haijafuzu Afcon kwa muda mrefu, lakini chini yangu imewezekana.

"Baada ya hapa nitarudi uingereza na kama nitaanza kufanya kazi nyingine nitafanya kwani kabla sijaondoka nilikuwa na kituo cha vijana nchini Uingereza na kama TFF, watakuwa tayari kufanya kazi na mimi katika kutafuta wachezaji vijana Ulaya nitakuwa tayari," alisema Ninje.