Matatizo ya Mo, Manji yalipima akili zetu

INAFURAHISHA sana, lakini wakati mwingine inatia huzuni. Baada ya kupotea kwa mmiliki mtarajiwa wa Simba, Mohammed Dewji, Mo, nilikuwa nasikia kile kile ambacho nilikuwa nasikia wakati tajiri wa Yanga, Yusuf Manji alipotiwa ndani kwa matatizo yake.

Mitandaoni na mitaani nilisikia mashabiki wa Yanga wakiwakejeli mashabiki wa Simba muda wao wa njaa umefika. Ni kama ambavyo mashabiki wa Simba walikuwa wana sherehe fulani hivi, kwa kile ambacho kilitokea Yanga wakati wa matatizo ya Manji.

Wanaongea utani? Hapana. Wengine walikuwa wanatoa mapovu. Ungeweza kusoma dhamira ya wanachokiongea kupitia sura zao. Kupitia maneno yao. Walikuwa wanawakilishia hisia za mioyo yao moja kwa moja.

Kuna tatizo la msingi katika klabu hizi. Tumekwama. Itachukua muda sana kwa klabu hizi kuwa taasisi. Labda Simba wakifanikisha mchakato wao ndio tutaweza kuelewa klabu hizi ni kubwa kuliko watu binafsi. Kuliko wanachama, kuliko mashabiki.

Kwa mfano, hata mashabiki wa Simba wenyewe walikuwa na wasiwasi kuhusu hali ya baadaye ya klabu yao baada ya Mo kutekwa. Sababu ni moja tu, mchakato mzima ulilenga kumpatia Mo timu. Sio kuwapatia wawekezaji wengine. Achilia mbali Mo binafsi, pia hawakugundua hata timu ingeweza kwenda kwa familia yake kama mwenyewe angetoweka kabisa.

Ni kweli inabidi tuonyeshe heshima kwa wale ambao wameonyesha nia ya kumiliki hizi klabu, lakini lazima tuzitengenezee miundombinu ya kudumu kuhakikisha hazipati matatizo pindi mmiliki au mtu mmoja anapopata matatizo.

Ni kama ambavyo mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich kwa sasa ana matatizo na serikali ya Uingereza na amenyimwa Visa ya kuingia England.

Hata hivyo, maisha ya Chelsea yanaendelea kama kawaida. Bila ya uwepo wake England, Chelsea imefukuza kocha, imeajiri, imenunua wachezaji. Maisha yanaendelea kama kawaida. Yaani kama kawaida.

Sahau kuhusu Roman, tajiri aliyeinunua Manchester United alifariki dunia Mei 2014, lakini mpaka leo familia yake bado inaendesha chama hilo. Ndivyo inavyotakiwa. Tujenge timu ambazo ni taasisi kupitia mifumo imara. Tatizo bado tunalenga watu tu.

Wakati mwingine ndani ya mfumo huu mpya wa umiliki, bado kuna mashabiki wataendelea kuwaona wamiliki kama vile ni wadhamini. Hili ni tatizo la msingi ambalo linasababisha tuwe na hofu pindi matajiri wanapopata matatizo.

Tutengeneze mfumo ambao timu zitamilikiwa na watu binafsi na zitakuwa kama taasisi imara ambazo zina misingi mikubwa kiasi mmiliki akipata matatizo basi hazitatetereka kwa kila kitu. Maisha yataendelea kama kawaida.

Bajeti ya klabu inabidi ifahamike. Wanafamilia wa mmiliki wa klabu wanapaswa kujua ambacho ndugu yao anakifanya katika timu. Lakini, thamani ya klabu pia lazima ijulikane ili mtu mwingine akijitokeza kununua wakati mmiliki ana matatizo isiwe dhambi.

Wenzetu ndio maana wanaishi bila ya wasiwasi. Klabu zao ni taasisi ambazo tayari zimewekwa katika njia sahihi. Ndio maana nimetoa mfano wa Abramovich na Grazer hapo juu. Tukiendelea kuishi kwa wasiwasi pindi mmiliki anapopata matatizo basi huo utakuwa sio umiliki, utakuwa ni ufadhili tu wa kawaida.

Wakati huu wanachama na mashabiki wakiwa wameanza kuelewa umuhimu wa klabu hizi kwenda katika nguvu za watu wachache nadhani ni wakati muhimu katika historia ya soka letu kuhakikisha klabu hizi hazipati matatizo tena pindi matajiri wanapopata matatizo.

Msingi mkubwa wa mfumo mzuri wa kuziendesha klabu hizi ni kuhakikisha unajengwa katika ukweli utajiri wa klabu hizi unatokana na uwingi wa mashabiki wake nchini na nje ya mipaka.

Wamiliki watakuwa wanatoa njia sahihi tu ya kuendesha klabu huku wakipata faida.

Kama mashabiki na wanachama bado hawataelewa hilo nadhani akili yao itaendelea kuwaona hawa kama wafadhili zaidi wakati wao ndio chanzo cha mapato na faida ambayo klabu inapata.

Kule Yanga mchakato unachelewa kwa sababu umelenga kumpatia timu mtu mmoja. Nadhani sio sahihi sana, ingawa tatizo kubwa ni wamejiweka katika kitanzi.

Mtu wanayemlenga ndiye huyo huyo ambaye anaweza kufanya mabadiliko kuelekea katika mchakato wa umiliki kwa sababu yeye ndiye mwenyekiti wa klabu mpaka sasa.