Mata: Manchester United tusiwadharau Club Brugge

Muktasari:

Kiungo huyo Mhispania, alisema makosa ya mara kwa mara yanaweza kuwagharimu katika mchezo huo wa raundi ya 32.

Kiungo Juan Mata amewaonya wachezaji wanzake wa Manchester United kwa kusema wanapaswa kutofanya makosa katika mchezo wa Europa Ligi dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji leo.

Kiungo huyo Mhispania, alisema makosa ya mara kwa mara yanaweza kuwagharimu katika mchezo huo wa raundi ya 32.

“Nadhani jambo muhimu kwetu ni kutofanya makosa, bao moja linaweza kukugharimu na kutupwa nje katika mashindano.Tunatakiwa kufanya kwa asilimia zote kile tunachopaswa kukifanya.

"Tunatakiwa kucheza kwenye kiwango chetu na sio vinginevyo. Haya mashindano ni tofauti na Ligi Kuu England ambayo unaweza kupoteza na ukajipanga na kupigania pointi katika michezo mingine," alisema.

Katika michezo iliyopita, Manchester United iliwahi kukutana na Club Brugge, ilikuwa 2015 katika Ligi ya Mabingwa na kuitwanga timu hiyo kutoka Ubelgiji kwa jumla ya mabao  7-1 katika michezo yote miwili yani nyumbani na ugenini.

Mata anaamini wanaweza kuvuka raundi hii na kutinga inayofuata katika mashindano hayo, " Ni timu nzuri na nina wakumbuka kwa sababu tuliwahi kucheza nao kwenye Ligi ya Mabingwa, wanauzoefu wa kutosha."

Michezo mingine ambayo inatarajiwa kuchezwa leo usiku ni pamoja na Olympiacos Piraeus dhidi ya Arsenal huku Wolves wao wakiwa na kibarua kizito mbele ya Espanyol.